Rais Macron aanza ziara rasmi ya siku tatu Ujerumani
26 Mei 2024Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kufanywa na rais wa Ufaransa nchini Ujerumani katika muda wa robo karne inapania kupunguza mvutano wa hivi karibuni kati ya Paris na Berlin na kutahadharisha juu ya ongezeko la siasa kali za mrengo wa kulia kuelekea uchaguzi wa bunge la Ulaya mwezi ujao.
Katika ziara hiyo ya siku tatu, Macron anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kihistoria wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili muhimu ya Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Macron asema vikosi vya usalam vitasalia New Caledonia
Uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani ambao unachukuliwa kama injini ya Umoja wa Ulaya haujakuwa mzuri katika siku za hivi karibuni hasa baada ya Macron kukataa kuondoa uwezekano wa kupeleka wanajeshi nchini Ukraine.
Kesho Jumatatu, Macron atasafiri hadi Dresden mji mkuu wa jimbo la Saxony katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki ambapo atatoa hotuba kuhusu masuala yanayoihusu Ulaya. Baadaye ataelekea mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Munster na kisha Meseberg, nje kidogo ya mji mkuu Berlin kwa mazungumzo na Kansela Olaf Scholz.