1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron atangaza hali ya hatari kisiwa cha New Caledonia

15 Mei 2024

Rais Emmauel Macron wa Ufaransa ametangaza hali ya hatari kwenye kisiwa cha bahari ya Pasifiki kilicho chini ya milki ya Ufaransa cha New Caledonia kufuatia siku ya pili ya ghasia.

https://p.dw.com/p/4ftaG
Kisiwa cha New Caledonia kilicho milki ya Ufaransa
Vurugu katika Kisiwa cha New Caledonia kilicho milki ya UfaransaPicha: MATHURIN DEREL/AFP

Rais Emmauel Macron wa Ufaransa leo ametangaza hali ya hatari kwenye kisiwa cha bahari ya Pasifiki kilicho chini ya milki ya Ufaransa cha New Caledonia kufuatia siku ya pili ya ghasia zilizosababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi mamia wengine.

Ghasia hizo zimechochewa na mageuzi ya katiba yanayoshinikizwa na Ufaransa kwenye kisiwa hicho kinachoendesha harakati za kutaka kujitenga.

Licha ya ulinzi mkali wa maafisa waliojihami kwa silaha nzito vurumai bado imetanda kote kwenye kisiwa cha New Caledonia kinachokutikana baina ya Australia na kisiwa cha Fiji. Taarifa ya ikulu ya Ufaransa, Elysee, imesema rais Macron ameonya kuwa machafuko zaidi yatakabiliwa na nguvu kubwa ya dola.

Maandamano na vurugu vyaendelea New Caledonia

Mageuzi yaliyozusha ghasia yanahusu kuwapatia kupiga kura watu walioishi kwenye kisiwa hicho kwa angalau miaka 10. Mapendekezo yanapingwa na kundi linalopigania uhuru ambalo linasema yatapunguza nguvu ya jamii ya wazawa katika ngazi za maamuzi.