Rais Erdogan kufanya ziara ya kwanza ya Misri leo
14 Februari 2024Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anatazamiwa kuwasili mjini Cairo leo hii kukutana na mwenzake wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, na kuhitimisha juhudi za maelewano ya muda mrefu kati ya viongozi hao wawili. Awali Jumatatu ofisi ya Erdogan ilisema katika mkutano huo watazunguzia jitihada ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, wakati shirika la habari la Uturuki, Anadolu likisema mkutano huo pia utahusu masuala ya uchumi, biashara, utalii, nishati pamoja na ulinzi. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kwa rais wa Uturuki nchini Misri tangu mwaka 2012. Nchi hizo mbili zilivunja mahusiano mwaka 2013 baada ya Sisi, aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Misri, kumuondoa madarakani Hayati Mohamed Morsi, mshirika wa Uturuki na sehemu ya vuguvugu la Udugu wa Kiislamu.