Raila atanganza kuwania kiti cha urais Kenya
10 Desemba 2021Basi la Azimio la umoja linaloongozwa na Raila Odinga, liling'oa nanga katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, uliochorwa rangi mpya za samawati na nyeupe za chama cha ODM. Aidha kila pembe ya uwanja huo yenye viti elfu sitini kulikuwa na mabango ya herufi za R zenye rangi ya chungwa, kuashiria jina la kiongozi huyo mwenye sifa ya kupigania demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya.
Kiongozi huyo ambaye alizuru taifa zima kabla ya kongamano la leo alibainisha hoja 10 ambazo ni mwarubaini kwa changamoto zinawakabili wakenya. Raila aliahidi kuwa serikali yake itatenga shilingi za Kenya bilioni mbili za kuwapa vijana kila mwaka. Kuhusu suala la afya,
Raila ameahidi kuwa kila Mkenya atakuwa na mpango wa bima ya afya, huku serikali yake ikiwalipia wale wasiojiweza. Huku Kenya ikiongoza kwa ukosefu wa nafasi za ajira Afrika Mashariki, Raila amesema kuwa, atahakikisha kuwa vijana wanapata kazi kwa kuboresha sekta ya jua kali. Hii itakuwa mara ya tano kwa Raila kuwania kiti cha urais.
"Nilipoongea na Wakenya nikawauliza niendelee au nisiendelee, nawajibu nitaendelea na tarehe nane tisa mwezi ujao, baba atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais.”, alisema Raila.
Wananaomuunga mkono Raila
Chama chake kitazindua mwongozo ambao utaelezea jinsi ya kukabiliana na ufisadi, deni kubwa la taifa, kujenga viwanda, kustawisha uchumi wa dijitali na jinsi ya kulinda mali ya watu binafsi. Viongozi wakuu wa Muungano wa Kenya moja-OKA, walisusia mkutano huo.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Musalia Mudavadi wa chama cha ANC na Moses Wetangula wa Ford Kenya, walidai kuwa na shughuli nyingine na kumtakia kila la kheri kwenye safari yake ya kuelekea Ikulu.
Kalonzo Musyoka wa Wiper alisafiri nchini Sudan kama mjumbe maalum wa amani. Hata hivyo Kiongozi wa chama cha Kanu Gidion Moi ambaye pia ni kiongozi wa OKA alihudhuria na kumpigia Raila Debe kuwa ana sifa zote za kuwa rais wa tano wa taifa la Kenya.
Upi msimamo wa Rais Kenyatta?
Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa wanashikilia kuwa viongozi hao wa OKA walisusia kuhudhuria hafla hiyo, kwani kwa kufanya hivyo kungeashiria kumuidhinisha Raila kuwa rais. Licha ya kuwa rais Uhuru Kenyatta kutokuepo baada ya kusafiri kwenda Tanzania kwa sherehe za miaka 60 tangu taifa hilo kujinyakulia uhuru, mawaziri sita na makatibu kadhaa walihudhuria, ishara ya kumwakilisha.
Aidha magavana 20 walihudhuria hafla hiyo. Tamko lake Raila linatia kikomo hali ya sintafahamu ambayo imekuwa ikizunguka hatma yake kisiasa.