Uchaguzi wa Rais wafanyika Nigeria
23 Februari 2019Rais Muhammadu Buhari amewataka wananchi wa Nigeria wajitokeze kwenda kupiga kura Jumamosi na ameahidi kwamba utakuwepo usalama wa kutosha. Katika uchaguzi huo ulioahirishwa wiki iliyopita Rais Buhari atapambana na mfanya biashara Atiku Abubakar ambaye hapo awali alikuwa makamu wa Rais. Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria wiki iliyopita iliahirisha uchaguzi huo wakati Wanigeria zaidi ya milioni 72 walipokuwa wanajitayarisha kwenda kupiga kura.
Akilihutubia taifa kwenye televisheni Rais Buhari amewataka Wanigeria wasiwe na wasiwasi na wawe na imani kwamba tume ya uchaguzi itatimiza jukumu lake. Naye mshindani wake kiongozi wa chama kikuu cha upinzani PDP Atiku Abubakar ametoa wito huo huo kwa wapiga kura.
Zaidi ya Wanigeria milioni 84 wameandikishwa kupiga kura kwenye taifa hilo lenye wakaazi milioni 190 la magharibi mwa Afrika. Lakini kwenye maeneo mengi ya kaskazini, ambako uasi wa kundi la Boko Haram umesababisha vifo vya zaidi ya watu 27,000 na kuwafanya mamilioni kuyakimbia makazi yao. Maelfu ya watu huenda wasiweze kushiriki kwenye uchaguzi wa Jumamosi Februari 23.
Kwa Wakaskazini waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na kundi la kigaidi la Boko Haram, hamu ya kupiga kura ni ndogo sana ingawa wanatarajia matokeo ya kura hiyo yatarudisha tena amani kwenye maeneo yaliyotawaliwa na matumizi ya nguvu.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE
Mhariri: Grace Kabogo