Qatar yataka misimamo ya wazi kuhusu mpango wa Gaza
4 Juni 2024Qatar ambayo imekuwa msitari wa mbele katika juhudi za usuluhishi kati ya Hamas na Israel, imesema waraka wa mapendekezo iliyouwasilisha kwa Hamas unakaribiana zaidi na misimamo ya kundi hilo pamoja na ile ya Israel, na kusisitiza kuwa laazima kuwepo na misimamo ya wazi kutoka pande hizo mbili kuelekea kusitisha vita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed Al-Ansari, amesema wanasubiri msimamo wa wazi wa Israel unaowakilisha serikali nzima ya Israel kuhusu pendekezo la Marekani.
"Na kama tulivyoona kutokana na kauli zilizotolewa jana na baadhi ya mawaziri wa Israel, hili bado halijatokea," alisema Al-Ansar.
"Nadhani mazungumzo yoyote juu ya kufikia makubaliano yanahitaji kwanza msimamo wa wazi kutoka kwa pande zote mbili kujibu maoni yaliopo mezani kwa sasa," aliongeza msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje.
Soma pia: Mkuu wa haki UN asema viwango vya vita vimekiukwa kikatili Gaza
Siku ya Ijumaa Biden alitoa pendekezo la awamu tatu kutoka Israel kwenda kwa Hamas ili kumaliza vita vya Gaza ambavyo vimeua makumi ya maelfu ya raia na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Pendekezo hilo linataka kusitishwa kwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, pamoja na ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza.
Hamas yakosoa kunyooshewa kidole
Hata hivyo afisa mwandamizi wa Hamas Sami Abu Zuhri, amekosoa miito ya Washington na mataifa mengine ya magharibi inayolitaka kundi hilo kukubali pendekezo hilo, akisema leo kwamba inaonekana kana kwamba wao ndiyo wamekwamisha juhudi za usitishaji vita.
Katika matamshi yalioripotiwa na chombo cha habari cha Hamas, Abu Zuhri amesema Israel haina nia ya kufikia makubaliano Gaza na ilikuwa inaendelea kucheza dana dana chini ya kivuli cha Marekani.
Matamshi yake yameonekana kuakisi mawazo ya Rais Joe Biden ambaye amenukuliwa akisema katika mahojiano aliofanyiwa Mei 28 na Jarida la Times, kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, huenda anakwamisha juhudi za kumaliza vita hivyo kwa sababu za kisiasa.
Soma pia: Zaidi ya nusu ya miundombinu yote Ukanda wa Gaza imeharibiwa
Biden aliongeza kuwa alitofautiana pakubwa na Netanyahu kuhusu mustakabali wa baada ya vita vya Gaza, na kusema Israel ilijihusisha na mwenendo "usiofaa" wakati wa vita hivyo vilivyochochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7.
Washirika wa Netanyahu waukubali mpango wa Biden
Wakati huohuo, mshirika mkubwa kabisaa wa Netanyahu serikalini, chama cha Shas, kimesema leo kuwa kitaunga mkono mpango wa kuwachiliwa kwa mateka kutoka kwa Hamas, hata kama hilo litahitaji kufumuliwa kwa mkakati wa Israel kuhusu vita vya Gaza.
Tamko hilo la Shas, ambacho ni chama chenye wafuasi wengi zaidi wa Kiorthodox kilicho na viti 11 kati ya 120 bungeni, limefuatia tamko sawa lililotolewa jana Jumatatu na Yitzhak Goldknopf, kiongozi wa chama cha pili mshirika katika muungano tawala, cha United Torah Judaism, kilicho cha vita saba.
Chanzo: Mashirika