1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Maafisa wa jeshi la polisi Kenya waburuzwa mahakamani

22 Agosti 2024

Maafisa watano wa polisi nchini Kenya walifikishwa mahakamani jana, wakituhumiwa kwa kumsaidia mshukiwa wa mauwaji na mahabusu wengine 12 kutoroka kwenye kituo kimoja cha polisi mjini Nairobi.

https://p.dw.com/p/4jla7
Kenya I Mtuhumiwa akiwa kizimbani
Mtuhumiwa akiwa katika kizimba cha mahakama nchini KenyaPicha: Simon Maina/AFP

Waendesha mashitaka wameiomba mahakama kuwazuilia polisi hao kwa wiki mbili ili kuwawezesha maafisa kukamilisha uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Maafisa hao wa polisi walikuwa kwenye zamu wakati wa tukio hilo la kutoroka jela kwa wafungwa hao. Waendesha mashitaka wameiomba mahakama muda zaidi ili kukusanya taarifa za mashahidi, kuchunguza kamera za usalama - CCTV na kuzichunguza simu za polisi hao.

Polisi ilisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa watu wa ndani waliwasaidia washukiwa kutoroka, na msako unaendelea kuwakamata tena waliotoroka.

Soma pia:Polisi Kenya yagundua miili ya watu 8 kwenye dampo la taka mjini Nairobi

Miongoni mwa waliotoroka ni Collins Jumaisi, aliyekamatwa Julai kuhusiana na mauaji ya karibu wanawake sita ambao miili yao ilipatikana ikiwa imefungwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa kwenye dampo.

Polisi inasema Jumaisi alikiri kuwauwa wanawake 42 akiwemo mkewe, lakini wakili wake aliiambia mahakama kuwa aliteswa na kulazimishwa kukiri tuhuma hizo. Waendesha mashitaka wanakanusha kuwa aliteswa.