Polisi wa mgodi walaumiwa kwa mauaji Tanzania
12 Juni 2024Polisi wanaolinda mgodi wa dhahabu wa North Mara nchini Tanzania wamehusishwa na mauaji ya watu wasiopungua sita na kujeruhi wengine kadhaa wakati wa mapigano tangu Februari mwaka huu.
Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, limeelezea kwenye ripoti iliyotoa hii leo, likizihimiza mamlaka za nchi hiyo kufanya uchunguzi huru na wa haraka.
Idadi inayoongezeka ya mauaji yanayohusishwa na mgodi wa dhahabu wa North Mara nchini Tanzania yanaonyesha mtindo unaotia wasiwasi wa kutoadhibiwa kwa unyanyasaji unaohitaji kushughulikiwa.
Soma pia: Tanzania yazindua Mgodi rasmi wa madini
Oryem Nyeko, mtafiti mkuu wa Tanzania katika shirika la Human Rights Watch, anasema "mamlaka za Tanzania hazipaswi kuvifumbia macho vifo hivi bali zinapaswa kuhakikisha kuwa waliohusika wanawajibishwa."
Maelezo ya ripoti ya Human Rights Watch
Polisi wamewatuhumu waliouawa na kujeruhiwa katika mgodi huo wa dhahabu kwa "kuvamia mgodi" na kufanya uchimbaji haramu ndani ya eneo la mgodi huo. Polisi wanawatuhumu wakaazi kwa wizi kutoka mgodi huo na maeneo yanayozunguka eneo lake la kutupia takataka.
Mwaka 2014, serikali ya Tanzania iliingia katika makubaliano na kampuni ya North Mara Gold Mine Limited kulinda mgodi huo wenye hadi polisi 110 wanaojulikana kama "polisi wa mgodi” pamoja na wanajamii, kwa utaratibu unaoendelea.
Mashirika ya haki za binadamu na wanajamii wameripoti kwamba katika miaka ya tangu makubaliano haya, maafisa wa polisi wamehusika kuwapiga, kuwapiga risasi, kuwatesa na kuwaweka kizuizini wakazi wa maeneo karibu na migodi na kutupa taka bila kufunguliwa mashtaka.
Lakini, licha ya madai hayo, shirika la Human rights watch linasema polisi hawajamkamata mtu yeyote kuhusiana na dhuluma hizi.
John Heche, mbunge wa zamani wa wilaya ya Tarime, ameliambia Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kuwa vitendo vya unyanyasaji wa polisi vimekithiri katika miaka ya hivi karibuni.
Amesema, "kwa miaka michache sasa, vifo hivi vimekuwa vikitokea, lakini haijawahi kutokea kwa kiwango hiki. Watu wanapigwa risasi karibu kila siku."
Human Rights Watch inasema mnamo tarehe 6 Mei mwaka huu, polisi walithibitisha kifo cha Emmanuel Nyakorenga, mkaazi wa kijiji cha Kewanja, eneo lililo karibu na mgodi huo.
Polisi walimtuhumu kuwa sehemu ya kundi lililowashambulia polisi kwa "silaha za jadi” walipozuiwa kuingia mgodini kinyume cha sheria.
Madhila ya wakaazi wanaoishi karibu na migodi
Tangu Mei 6, wakaazi wa huko wameripoti vifo vya takribani watu wengine watatu katika eneo hilo. Siku moja baada ya kifo cha Nyakorenga, wakaazi waliripoti kwamba walipata mwili wa mtu asiyejulikana katika eneo la kutupa takataka za mgodi huo nje ya eneo la mgodi.
Mnamo Mei 22, vyombo vya habari viliripoti kuwa, Babu Christopher Iroga, mkaazi wa kijiji cha Mjini Kati, na July Mohali, mkaazi wa kijiji cha Nyangoto, waliuawa wakati wa mapambano na polisi. Polisi waliwashutumu wanaume hao kwa kuiba kwenye mgodi huo.
Soma pia: Kenya: Watu watano wafariki katika ajali kwenye mgodi wa dhahabu
Mwaka 2022, Watanzania 21 waliishtaki kampuni ya Barrick Gold katika mahakama ya Canada, wakiishutumu kwa kuhusika na mauaji ya kiholela na kupigwa kwa wakaazi kunakofanywa na polisi waliopewa kazi ya kuulinda mgodi huo.
Walidai kuwa kampuni hiyo iliwageuza polisi wanaofanya kazi ndani na karibu na mgodi huo "kuwa kikosi cha usalama cha kibinafsi na chenye silaha nzito." Kesi hii imepangiwa kuanza kusikilizwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Nyeko, mtafiti mkuu wa shirika hilo nchini Tanzania anasema, "Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha uchunguzi huru na usio na upendeleo kuhusu unyanyasaji huu ili waathiriwa na familia zao wapate haki."