1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pfizer na BioNTech: Chanjo ya Covid-19 ina ufanisi wa 90%

10 Novemba 2020

Chanjo inayotengenezwa kwa pamoja kati ya kampuni za Pfizer kutoka Marekani na BioNTech ya Ujerumani, imedhihirisha ufanisi wa asilimia 90 katika kuzuwia maambukizi ya covid-19, kulingana na majaribio ya awamu ya tatu.

https://p.dw.com/p/3l5kk
Coronavirus | Impfstoff | Pfizer
Picha: Zeljko Lukunic/PIXSELL/picture alliance

Hayo yanajiri wakati Brazil ikisitisha majaribio ya chanjo ya kampuni ya Kichina ya Sinovac, ikielezea tukio baya lilitokea wakati wa majaribio ya chanjo hiyo.

Mamlaka ya afya ya Brazil, Anvisa, ilisema Jumatatu kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 29, lakini haikubainisha iwapo lilitokea nchini humo au katika taifa jengine. Pia haikutoa kiashiria chochote juu ya hadi lini usitishaji huo utadumu.

Soma pia:Mkuu wa WHO aonya dhidi ya 'utaifa wa chanjo' 

Majaribio hayo ni moja ya majaribio matatu makubwa ya hatua ya mwisho yanayofanyika kwa chanjo ya Sinovac. Chanjo hiyo imekabiliwa na utata nchini Brazil, baada ya rais Jair Bolsonarokuipuuza na kusema inakosa uaminifu.

Virusi vya Corona vinaendelea kuisumbua Ujerumani

Pigo hilo kwa juhudi za Sinovac ni kinyume cha habari njema kutoka kampuni za dawa za Pfizer ya nchini Marekani na BioNTech ya Ujerumani, zilizosema kuwa chanjo yao ya Covid-19 ina ufanisi wa zaidi ya asilimia 90 kwa mujibu wa matokeo ya majaribio ya awali.

Soma pia: J&J yasitisha majaribio ya chanjo baada ya mtu kuugua

"Wengi wenu mmesikia habari njema. Zimekuwa katika habari za kitaifa. Utafiti unaoendelea unaonesha ufanisi wa asilimia 90 na zaidi, hilo linamaanisha kuwalinda wagonjwa waliochanjwa na kuwazuwia kupata maambukizi ya covid-19," alisema John Burkhat, makamu wa rais wa Pfizer anaehusika na usalama wa dawa.

Symbolbild Corona Impfstoff Biontech und Pfizer BNT162bt
Kampuni za Pfizer na BioNTech zinasema chanjo yao ina ufanisi wa asilimia zaidi ya 90.Picha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Hakuna mashaka makubwa ya kiusalama

Taarifa kutoka kampuni hizo mbili ndiyo utoaji wa kwanza wa taarifa za mafanikio kutokana na majaribio makubwa ya chanjo ya covid-19. Kulingana na ripoti zao, hawakugundua mashaka yoyote makubwa ya kiusalama yanayohusishwa na chanjo hiyo. Watafiti wanaamini athari ya chanjo hiyo haitadumu kwa muda mfupi.

Soma pia:Majaribio ya chanjo ya corona kuanza tena

Iwapo itathibitishwa, chanjo ya Pfizer na BioNTech itakuwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya janga la virusi vya corona. Afisa Mtendaji Mkuu wa BioNTech Ugur Sahin alisema wana matumaini kwamba athari ya chanjo hiyo inaweza kudumu kwa angalau mwaka mmoja.

Deutschland Mainz | BioNTech SE | Pressebilder
Chanjo ya majaribio ya BNT162 kutoka kampuni ya BioNTech.Picha: BioNTech SE 2020, all rights reserved

Rais mteule wa Marekani Joe Biden alikaribisha matokeo hayo ya matumaini kutoka majaribio ya chanjo, lakini alionya kwamba utolewaji wa chanjo kwa watu wengi ulikuwa mbali bado kwa miezi kadhaa, na kuuhimiza umma wa Marekani kuendelea kuvaa barakoa na kuweka umbali kati ya mtu na mtu.

Soma pia:Chanjo ya COVID-19 majaribio yasitishwa

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn alisema Umoja wa Ulaya utasubiri kuidhinisha chanjo hiyo hadi zitakapotolewa taarifa za usalama za hatua za mwishoni mwa majaribio, ili kuhakikisha uaminifu mpana zaidi iwezekanavyo wa chanjo hiyo.

Vyanzo: rtre,aptn,dw