J&J yasitisha majaribio ya chanjo baada ya mtu kuugua
13 Oktoba 2020Idadi ya kesi zilizothibitishwa za maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani imeongezeka kwa watu 4,122 hadi jumla ya watu 329,453, data kutoka katika taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch, zimeonesha hii leo. Idadi ya watu waliofariki hadi sasa imepanda kwa watu 13 hadi watu 9,634, data hizo zimeonesha. Soma pia: Maambukizi ya Corona yaongezeka Ulaya na Amerika Kusini
Utafiti wa hatua ya juu uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Johnson & Johnson wa chanjo ya COVID-19 umesitishwa kwa muda wakati kampuni hiyo inachunguza iwapo mmoja wa watu waliojitolea kushiriki katika chanjo hiyo, alipata ugonjwa ambao haukuweza kupatiwa maelezo kwa haraka, kama unahusiana na chanjo hiyo.
Mataifa ya Ulaya leo yamekubaliana kuhusu mbinu za pamoja za kuratibu vizuwizi vya usafiri kutokana na janga la virusi vya corona, katika juhudi za kufikisha mwisho sheria za kitaifa za kuumba umba ambazo zimejitokeza wakati huu wa janga.
Nchini Ufaransa baraza la mawaziri litakutana leo kujadili hatua zaidi za kupambana na janga la virusi vya corona, amesema naibu waziri wa nyumba na makaazi Emmanuelle Wargon. Alipoulizwa juu ya uwezekano wa kuweka marufuku ya kutoka nje wakati wa usiku katika miji kama paris ambako kesi za maambukizi zinaongezeka, alirudia matamshi ya waziri mkuu Jean castex kuwa hatuna fursa itakayowekwa kando. Soma pia: Trump arejea kwenye kampeni baada ya kupona COVID-19
Serikali ya Uingereza nayo huenda ikaweka vizuwizi vikali zaidi kuliko vya hivi sasa iwapo wimbi la pili la maambukizi litaendelea katika maeneo yaliyoathirika zaidi. Waziri mkuu Boris Johnson alitangaza mfumo mpya wa vizuwizi kwa England jana Jumatatu, ambapo Liverpool na eneo lake la Merseyside liliwekwa katika kiwango cha juu cha eneo la hatari, na vilabu vya pombe vilifungwa kuzuwia ongezeko la maambukizi ya COVID-19.
Serikali ya Italia inaimarisha hatua zake dhidi ya kusambaa kwa ugonjwa huo wa COVID-19, kwa kupiga marufuku hafla za watu binafsi na marufuku ya watu kuendelea kuwa katika mabaa na mikahawa nyakati za usiku.
Huko Urusi idadi ya kesi za maambukizi ya virusi vya corona imepanda kwa watu 13,868 leo, ikiwa ni rekodi mpya ya idadi kwa siku tangu kuanza kwa janga hili mapema mwaka huu. India nayo imeripoti maambukizi mapya 55,342 leo , ikiwa ni ya chini kwa siku tangu katikati ya mwezi Agosti.
dpae / rtre / ape