1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya virusi vya corona yaongezeka duniani

12 Oktoba 2020

Taasisi ya Robert Koch nchini Ujerumani imethibitisha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini humo kufikia 325,331. Mataifa mbali mbali pia yanaweka mikakati mipya ya kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3jmwd
China | Covid-19 | Coronavirus -Test
Picha: Noel Celis/AFP/Getty Images

Helge Braun, msaidizi wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amesema nchi hiyo inapaswa kuthibiti idadi ya watu wanaoruhusiwa kukusanyika na kuzuia safari zisizo za laazima huku nchi hiyo ikiendelea kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona. Braun ameliambia shirika la habari la umma ARD nchini humo kwamba laazima hatua kali zaidi zichukuliwe katika maeneo ambayo maambukizi yanaenea kwa haraka kama vile sherehe na kwa bahati mbaya usafiri pia.

Nchini Uingereza, waziri mkuu Boris Johnson, leo anatarajiwa kutangaza mikakati mipya ya kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona na kunuia kushirikiana zaidi na viongozi katika maeneo yalioathirika zaidi nchini humo. Eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo limeathirika pakubwa na kuzuka upya kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vimesababisha kuwekwa sheria ya watu kutotoka katika maeneo yao huku wanafunzi wakirejea shuleni na vyuoni kote nchini humo.

Jean Castex Frankreich Politik
Jean Castex- Waziri mkuu wa UfaransaPicha: picture-alliance/abaca/M. Baucher

Naye waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex  ameonya kuwa mamlamka nchini humo huenda zikalazimika kuweka sheria mpya ya watu kutoruhusiwa kutoka katika maeneo yao katika juhudi za kukabiliana na visa vinavyoongezeka vya maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vinatatiza utoaji huduma za afya katika hospitali nyingi.

Katika mahojiano na kituo cha redio cha Franceinfo, Castex alisema kuwa iwapo katika muda wa wiki mbili zijazo viashiria vya janga la corona vitaongezeka, vyumba vya kushughulikia wagonjwa mahututi kujaa zaidi ya inavyotarajiwa, hatua zaidi zitachukuliwa. Na alipoulizwa iwapo hatua za watu kubaki majumbani na kufungwa kwa biashara zinaweza kuchukuliwa, aliongeza kuwa hakuna lisilowezekana kufanyika.

Nchini India, idadi kamili ya maambukizi ya corona iliongezeka kwa visa 66,732 katika muda wa saa 24 kufikia maambukizi milioni 7.12 leo asubuhi. Haya ni kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa wizara ya afya nchini humo. Wizara hiyo imeongeza kuwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 viliongezeka kwa 816 kufikia 109,150.

Israel nayo jana ilifungua kituo kipya cha kutibu maambukizi ya virusi vya corona kinachosimamiwa kwa ushirikiano na kitengo cha matibabu cha jeshi la nchi hiyo , hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa kitengo hicho cha jeshi, hali inayolenga kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za matibabu unaokabiliwa na changamoto. Mkuu wa kitengo cha kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona jeshini Ariel Furer, amesema hii ni mara ya kwanza kwa kitengo hicho cha kijeshi kufanya kazi katika hospitali za umma.