1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa abariki mahusiano ya jinsia moja yasiofanana na ndoa

27 Desemba 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis ameridhia mapadri kubariki wapenzi wa jinsia moja, katika mabadiliko ya sera yanayonuwiwa kulifanya Kanisa kuwa shirikishi zaidi lakini likibakisha marufuku ya ndoa za jinsia moja

https://p.dw.com/p/4aLLF
Vatikan Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.Picha: GUGLIELMO MANGIAPANE/REUTERS

Lakini wakati taarifa ya Vatikani ilitangazwa na baadhi ya watu kama hatua ya kuvunja ubaguzi katika Kanisa Katoliki, baadhi ya watetezi wa LGBTQ+ walionya inasisitiza wazo la kanisa hilo kwamba wapenzi wa jinsia moja wanabaki kuwa wa chini ya wale wanaoshiriki mahusiano ya jinsia tofauti.

Waraka kutoka ofisi ya mafundisho ya Vatikani unafafanua barua ambayo Francis alituma kwa makadinali wawili wahafidhina ambayo ilichapishwa mnamo Oktoba. Katika jibu hilo la awali, Francis alipendekeza baraka kama hizo zingeweza kutolewa chini ya hali fulani ikiwa baraka hizo hazichanganywi na ibada ya ndoa.

Waraka huo mpya unarudia sharti hilo na kulifafanua kwa kina, ukithibitisha tena kwamba ndoa ni muungano wa maisha yote kati ya mwanamume na mwanamke. Na unasisitiza kwamba baraka zinazohusika hazipaswi kuhusishwa na sherehe yoyote maalum ya Kikatoliki au huduma ya kidini na haipaswi kutolewa kwa wakati mmoja kama sherehe ya ndoa. Zaidi ya hayo, baraka hizo haziwezi kufuata desturi iliyowekwa au hata kuhusisha mavazi na ishara zinazotumika katika arusi.

Soma pia:Papa ashutumu ushoga kufanywa uhalifu 

Lakini unasema maombi ya baraka hizo kwa wapenzi wa jinsia moja hayafai kukataliwa. Unatoa ufafanuzi mpana na wa kina wa neno "baraka" katika maandiko kusisitiza kwamba watu wanaotafuta uhusiano upitao maumbile na Mungu na kutafuta upendo na rehema yake haipaswi kuwekewa kiwango kisichowezekana cha maadili ili kuupokea.

Vatikan| Papa Francis na Kadinali Victor Manuel Fernandez
Waraka wa Kanisa unasisitiza kuwa mahusiano ya jinsia moja bado ni dhambi.Picha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP/Getty Images

"Kwa maana, wale wanaotafuta baraka hawapaswi kuhitajika kuwa na ukamilifu wa maadili," ulisema waraka huo. "Hakuna nia ya kuhalalisha kitu chochote, lakini ni kufungua maisha ya mtu kwa Mungu, kuomba msaada wake ili kuishi vizuri zaidi, na pia kumwomba Roho Mtakatifu ili tunu za Injili ziweze kuishi kwa uaminifu zaidi," uliongeza.

Waraka huo unaashiria hatua ya hivi karibuni zaidi ya papa ambaye amefanya kuwakaribisha Wakatoliki wa LGBTQ+ kuwa alama mahususi ya upapa wake. Kuanzia jibu lake la 2013, "Mimi ni nani kuhukumu?" kuhusu kasisi anayedaiwa kuwa shoga, hadi maoni yake ya 2023 kwa shirika la Associated Press kwamba "Kuwa ushoga si kosa," Francis amejitofautisha na watangulizi wake wote kwa ujumbe wake wa kukaribisha.

"Umuhimu wa habari hizi hauwezi kusisitizwa vya kutosha," alisema Francis DeBernardo wa New Ways Ministry, ambayo inaunga mkono Wakatoliki wa LGBTQ+. "Ni jambo moja kuidhinisha rasmi baraka kwa wapenzi wa jinsia moja, ambazo tayari alikuwa ameziruhusu kichungaji, lakini kusema kwamba watu hawapaswi kufanyiwa "uchambuzi wa kina wa maadili" ili kupokea upendo na huruma ya Mungu ni hatua muhimu zaidi."

Soma pia:Mamia ya Waislamu waandamana Kenya kupinga ushoga 

Vatikani inashikilia kuwa ndoa ni muungano usioweza kuvunjika kati ya mwanamume na mwanamke. Matokeo yake, kwa muda mrefu imekuwa ikipinga ndoa za watu wa jinsia moja na inachukulia vitendo vya ushoga kuwa "upotofu." Hakuna kitu katika waraka mpya kinachobadilisha mafundisho hayo.

Na mnamo 2021, Kusanyiko la Mafundisho ya Imani la Vatikani lilisema waziwazi kwamba kanisa haliwezi kubariki miungano ya wanaume wawili au wanawake wawili kwa sababu "Mungu hawezi kubariki dhambi."

Tangazo hilo la 2021 lilizua kilio na kuonekana kumshangaza Francis, ingawa kimsingi alikuwa ameidhinisha uchapishaji wake. Punde baada ya kuchapishwa, alimwondoa ofisa aliyehusika nalo na kuanza kuweka msingi wa kuibadilisha.

Idhini ya Papa wapenzi wa jinsia moja ina maana gani?

Katika waraka mpya, Vatikani ilisema kanisa lazima liepuke "mipango ya mafundisho au ya kinidhamu haswa inaposababisha ubinafsi wa kimabavu ambapo badala ya kueneza injili, mtu huchambua na kuwaainisha wengine." Ulisema hatimaye, baraka ni juu ya kusaidia watu kuongeza imani yao kwa Mungu. "Ni mbegu ya Roho Mtakatifu ambayo inapaswa kukuzwa, sio kuzuiwa," ulisema waraka huo.

Soma pia: Vatikani yakasirishwa na mwenendo wa shirika la kitawa

Ulisisitiza kwamba watu walioko katika miungano "isiyo ya kawaida" ya ngono nje ya ndoa, wawe mashoga au jinsiy tofauti, wako katika hali ya dhambi. Lakini ulisema hilo lisiwanyime upendo au huruma ya Mungu. "Hata wakati uhusiano wa mtu na Mungu umegubikwa na dhambi, anaweza kuomba baraka kila wakati, akinyoosha mkono wake kwa Mungu,” waraka huo ulisema.

Hisia mchanganyiko kutoka kwa viongozi wa Kanisa

Kasisi James Martin, ambaye anatetea kukaribishwa zaidi kwa Wakatoliki wa LGBTQ+, alisifu waraka huo mpya kama "hatua kubwa mbele" na "mabadiliko makubwa" kutoka sera ya Vatikani ya 2021. "Pamoja na makasisi wengi wa Kikatoliki, sasa nitafurahi kuwabariki marafiki zangu katika ndoa za jinsia moja," alisema katika barua pepe.

Wanamapokeo, hata hivyo, walikasirishwa. Mwanablogu wa jadi Luigi Casalini wa Messa katika blogu ya Kilatino (Misa ya Kilatini) aliandika kwamba waraka huo ulionekana kuwa aina ya uzushi. "Kanisa linaporomoka," aliandika.

Mwanatheolojia wa Chuo Kikuu cha Notre Dame Ulrich Lehner pia alikuwa na wasiwasi, akisema ungezusha tu machafuko na unaweza kusababisha mgawanyiko katika kanisa.

"Tamko la Vatikani, kwa maoni yangu, ni tangazo la bahati mbaya zaidi katika miongo kadhaa," alisema katika taarifa yake. "Zaidi ya hayo, baadhi ya maaskofu wataitumia kama kisingizio cha kufanya kile ambacho waraka huo unakataza waziwazi, hasa kwa vile Vatikani haijawazuia hapo awali. Ni-na sipendi kusema hivyo - mwaliko wa mifarakano."

Soma pia:Papa Francis akemea unyanyasaji wa kingono unaofanywa na makasisi Ureno 

Ramón Gómez, anayesimamia haki za binadamu katika Vuguvugu la ushirikishwaji na Uhuru wa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini Chile, alisema kauli hiyo ni hatua ya kukomesha ubaguzi katika kanisa na inaweza kuwasaidia wana LGBTQ+ katika nchi ambazo hata ndoa za kiraia si halali.

Ujerumani |Kanisa Katoliki labaariki wapenzi wa jinsia moja.
Mchungaji wa Kikatoliki akiwabaariki wapenzi wa jinsia moja katika mji wa Cologne, nchini Ujerumani, Mei 10, 2021. Mkuu wa Kanisa Katoliki Ujerumani ameunga mkono tamko la Kanisa kuhusu kuwabaariki wapenzi wa jinsia moja.Picha: Andreas Rentz/Getty Images

Nchini Ujerumani, makasisi mmoja mmoja wamekuwa wakiwabariki wapenzi wa jinsia moja kwa miaka, kama sehemu ya mwelekeo wa maendeleo katika kanisa la Ujerumani. Mnamo Septemba, makasisi kadhaa wa Kikatoliki walifanya sherehe ya kubariki wanandoa wa jinsia moja nje ya Kanisa Kuu la Cologne, katika hatua ya kumpinga askofu mkuu wa jiji hilo, Kadinali Rainer Maria Woelki.

Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Ujerumani alikaribisha waraka huo. "Hii ina maana kwamba baraka inaweza kutolewa kwa wanandoa ambao hawana fursa ya kuoana kanisani, kwa mfano kutokana na talaka, na wapenzi wa jinsia moja," Askofu Georg Baetzing alisema katika taarifa yake. "Utendaji wa kanisa unajua aina mbalimbali za baraka. Ni vyema kwamba hazina hii ya aina mbalimbali za maisha sasa inainuliwa."

Soma pia:Museveni asaini sheria ya mapenzi ya jinsia moja 

Nchini Marekani, John Oesterle, kasisi wa Kikatoliki na kasisi wa hospitali ya Pittsburgh, alisema huenda makasisi wengi hawatakuwa tayari kutoa baraka hizo, lakini alikaribisha hatua ya Francis.

"Nadhani papa amejifunza kukubali watu kama Mungu alivyowaumba," alisema Jumatatu. "Nilipokuwa mdogo, dhana ilikuwa kwamba Mungu alimfanya kila mtu kuwa sawa. Tulichojifunza si kweli. Katika kuwapokea watu kama Mungu alivyowaumba, na ikiwa mafundisho ya msingi ya Yesu ni tunapaswa kupendana na kutumikiana katika jumuiya, nadhani hilo ndilo linalompa Papa Francis uwazi wa uwepo wa Mungu katika mahusiano hayo."

Sheria mpya wa kudhibiti kubadili jinsia yaja Urusi