1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obasanjo aingia kati kuwapatanisha Ruto, Raila

31 Julai 2023

Juhudi za upatanishi nchini Kenya zimechukua sura mpya baada ya kinara wa upinzani, Raila Odinga, na Rais William Ruto kuridhia mazungumzo, kufuatia vikao kati yao na rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.

https://p.dw.com/p/4Uahl
Kenia Wahlen Raila Odinga William Ruto
Picha: AFP

Akiwa ziarani katika eneo la Pwani mwishoni mwa wiki, Rais Ruto alithibitisha kufanya mazungumzo na Rais Obasanjo na Odinga kusaka suluhu ya mkwamo wa kisiasa uliopo.

Hata hivyo, Ruto alisisitiza kuwa suala la usalama wa taifa na sera za uchumi ni wajibu wa serikali, jambo lililoashiria kuwa halitakuwemo kwenye ajenda za maridhiano.

Soma zaidi: Mahakama ya rufaa yaruhusu utekelezaji wa sheria ya fedha, 2023
Ruto: Niko tayari kukutana na Odinga wakati wowote

Taarifa kutoka vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo zilisema kuwa mahasimuj hao wawili wamekubali kutafuta suluhu ya mivutano iliyopo.

Pande zote mbili ziliafikiana kuunda kamati mpya ya wajumbe kumi wakiwemo wasiokuwa wabunge.

Lakini Spika wa Baraza la Seneti kutoka muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto, Amason Kingi, ni miongoni mwa wale ambao hawana imani na harakati hizo kwani "upinzani haujamtambua rasmi Rais Ruto kuwa ni kiongozi wa taifa."

Azimio waelezea msimamo wao

Kwa upande wao, viongozi wa upinzani wa Azimio la Umoja walisisitiza kuwa azma yao ni "kulinda maslahi ya Wakenya na wala sio kujitengea nafasi za kazi."

Äthiopien Addis Abeba 2021 | H.E. Chief Olusengu Obasanjo, AU-Wahlbeobachter
Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.Picha: Minasse Wondimu Hailu/Anadolu Agency/picture alliance

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili, viongozi hao walikiri kuwa kinara wao, Odinga, alikutana na Rais Ruto kuandaa mikakati ya vikao vya suluhu.

Wakati huo huo, Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema viongozi wa upinzani wa Azimio la Umoja waliopokonywa walinzi watalazimika kusubiri kwa miezi mitatu kabla kurejeshewa. 

Soma zaidi: Wafuasi wa upinzani wa Azimio la Umoja nchini Kenya wafanya maombolezi rasmi kote nchini

Kenya yahitimisha siku ya tatu ya maandamano

Wiki iliyopita, kiongozi wa upinzani kwenye Baraza la Seneti aliitaka Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Ulinzi kubainisha hatma ya walinzi walioondelewa.

Viongozi hao walipokonywa walinzi kabla ya wimbi jipya la maandamano ya kuishinikiza serikali kushusha gharama za maisha kuanza wiki iliyopita.

Yote hayo yakiendelea, Seneta wa Busia, Okiya Omutata, amewasilisha kesi kwenye mahakama ya juu ili kutaka  uamuzi wa mahakama  ya rufaa ulioruhusu utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 kubatilishwa.

Imeandaliwa na Thema Mwadzaya/DW Nairobi