1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yangoja uvamizi wa kijeshi wa ECOWAS

7 Agosti 2023

Niger inasubiri kwa tahadhari hatua za Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) baada ya watawala wa kijeshi kupuuza muda wa mwisho uliowekwa na jumuiya hiyo wa kumrejesha madarakani rais aliyepinduliwa.

https://p.dw.com/p/4Uqlb
Niger, Niamey | Kundgebung von Anhänger der Putschisten
Picha: Mahamadou Hamidou/REUTERS

Jumuiya hiyo ilitoa muda wa wiki moja hadi siku ya Jumapili (6 Julai) kwa wanajeshi walioipindua serikali nchini Niger kurejesha madaraka kwa Rais Mohamed Bazoum au wakabiliwe na hatua kali ikiwemo uingiliaji kati kijeshi.

Soma zaidi: Niger yafunga anga ikihofia uvamizi wa ECOWAS

ECOWAS imesema itatoa taarifa rasmi juu ya hatua inazolenga kuchukuwa baada ya majenerali kukaidi shinikizo la kimataifa la kuondoka madrakani tangu walipofanya mapinduzi mnamo Julai 26. 

Siku ya Jumapili utawala huo wa kijeshi ulitangaza kuifunga anga ya nchi hiyo kwa muda usiojulikana, uamuzi unaotowa ishara ya kuongezeka wasiwasi wa ECOWAS kutuma kikosi cha kijeshi kuwalazimisha kukabidhi madaraka.