1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nia ya Uganda kuondoa wanajeshi DRC yazusha maoni mseto

Daniel Gakuba
18 Mei 2022

Nia iliyotangazwa na kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ya kutaka kuondoa majeshi yake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwishoni mwa mwezi Mei imepokelewa kwa maoni mseto.

https://p.dw.com/p/4BSfd
Afrika Uganda Edward Katumba Wamala
Kamanda Mkuu wa jeshi la Uganda (UPDF) Jenerali Edward Katumba Wamala (katikati) akiwa na makamanda wa jeshi la Kongo mjini Beni mwanzoni mwa Mei 2022.Picha: AFP via Getty Images

Dhamira hiyo ya Uganda ilitangazwa kupitia ujumbe wa Twitter na kamanda wa majeshi ya nchi kavu wa nchi hiyo Jenerali Muhoozi Kainerugaba. Jenerali huyo aliandika kuwa iwapo marais wa nchi hizo mbili hawatafikia makubaliano ya hatma ya operesheni Shujaa mashariki mwaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,  wanajeshi  wapatao 4,000 wa Uganda wataondolewa.

Soma zaidi: Idadi ya waliokufa kwenye shambulio nchini Congo yafikia 8

Operesheni Shujaa inayoendeshwa na majeshi ya mataifa hayo mawili mashariki mwa Kongo ililenga kuwatokomeza wapiganaji wa kundi la Allied Democratic Forces, ADF. Kundi hilo ambalo asili yake ni Uganda na limekuwa likiwahangaisha raia mashariki mwa Kongo kwa muda mrefu.

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Waasi wa ADF wamesababisha adha kubwa kwa wakaazi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Kipindi cha operesheni hiyo kilikuwa miezi sita na kinakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei pakiwa na mafanikio kadhaa, lakini ambayo hayajaridhisha pande zote mbili.

Kongo ingependa UPDF iendelee na kazi

Mamlaka za Kongo zimenukuliwa zikisema ni mapema mno kwa Uganda kuondoa majeshi yake. Hii inafuatia ujumbe wa Twitter wa kamanda wa majeshi ya nchi kavu wa Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba hapo jana kwamba kulingana na mkataba wa awali wa operesheni hiyo muda wao unaelekea ukingoni.

Katika ujumbe wake, Jenerali Muhoozi ameongezea kusema kuwa mashauriano na maelekezo kati ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye ni baba yake pamoja na Felix Tshisekedi, rais wa Kongo ndiyo yataelezea ni hatua zipi zitachukuliwa.

Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Operesheni za pamoja kati ya majeshi ya Kongo na Uganda zinaelezwa kuleta mafanikio kiasi fulaniPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Soma zaidi: Uganda kuwarejesha wanajeshi wake walioko Sudan Kusini 

Waziri wa Habari wa Kongo Patrick Muyaya ambaye pia ni msemaji wa serikali naye amenukuliwa akisema kuwa operesheni hiyo imefanikiwa kwa kiwango fulani kuwakabili wapiganaji wa ADF, na kuongeza lakini kuwa itakuwa bora tathmini ifanyike ili kubaini kama wametimiza malengo ya awali ya operesheni hiyo.

Wakimbizi wasema bado hakuna uthabii nyumbani kwao

Kulingana na wadadisi pamoja na raia na wakimbizi kutoka Kongo, hali thabiti ya amani na utulivu bado haijashuhudiwa katika. Takwimu za shirika la Umoja Mataifa linalowashughulikia wakimbizi, UNHCR zinaonyesha kuwa zaidi ya raia 30,000 wa mashariki mwa Kongo wamekimbilia usalama wao Uganda tangu mwezi Januari mwaka huu.

Soma zaidi: DRC: Wito watolewa FARDC na UPDF kuungana kukabili ADF-Nalu 

Kufuatia hatua ya Kongo kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uganda na mataifa mengine wanachama ikiwemo Rwanda na Burundi yanataka kuwepo na amani mashariki mwa nchi hiyo ili kujenga mazingira bora ya kibiashara na uwekezaji.

 

Mwandishi: Emmanuel Lubega/DW Kampala