1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani bingwa wa Afrika?

19 Julai 2019

Afrika itakuwa na bingwa mpya wa kandanda Ijumaa. Algeria wanakabiliana na Senegal katika fainali itakayochezwa mwendo wa saa nne usiku saa za Afrika Mashariki huko Cairo nchini Misri.

https://p.dw.com/p/3MKRZ
Afrika Cup 2019 | Riyad Mahrez und Sadio Mane
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Schalit

Algeria ndio imekuwa timu bora katika kinyang'anyiro hiki hadi kufikia sasa, ilishinda mechi zake zote za kundi lililojumuisha wapinzani wao wa leo Senegal. Kenya na Tanzania pia walikuwa katika kundi hilo. Katika mechi ya mtoano ya raundi ya 16 iliwazaba Guinea 3-0 halafu katika robo fainali wakawazidi kete Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti.

Katika nusu fainali walipambana na Nigeria na wakawazidi nguvu dakika ya mwisho. Nahodha na mchezaji nyota wa hao "Mbweha wa Jangwani" kama wanavyoitwa kwa jina la utani, Riyad Mahrez, alifunga goli la ushindi kupitia mkwaju wa frikiki.

Senegal hawajashinda ubingwa wa Afrika na wamefika fainali baada ya miaka 17

Senegal kwa jina la utani wanaitwa "Simba wa Teranga". Katika kundi lao walipoteza mechi moja tu dhidi ya Algeria ila walishinda mechi dhidi ya Tanzania na Kenya na kufuzu katika raundi ya mtoano ambapo walishinda mechi zao zote kwa bao moja kuanzia hapo, waliwapeleka nyumbani Uganda Benin na Tunisia.

Africa Cup 2019 | Senegal v Algerien
Algeria walishinda mechi ya kundi dhidi ya Senegal 1-0Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Hii ni mara ya kwanza Senegal wanafika fainali ya mashindano haya baada ya miaka 17. Aliou Cisse ni kocha wao.

"Miaka kumi na saba ni muda mrefu sana. Idadi kubwa ya wachezaji wetu wakati huo walikuwa ni watoto bado. Kulikuwa na machozi mengi wakati huo. Lakini tumerudi tena katika fainali na hatutaki kuishia hapa tu. Kikosi hiki kina talanta sana," alisema Cisse.

Algeria kwa upande wao wanatafuta kuebuka mabingwa kwa mara ya pili baada ya kutawazwa taji hilo 1990. Kocha wao Djamel Belmadi lakini anasema walio na nafasi nzuri ni Senegal.

Makocha wote wawili wanajuana vyema na walikulia Ufaransa

"Bila shaka tunaweza kuipoteza mechi hii kwasababu tunacheza na wapinzani ambao wameshawahi kufika fainali na wanaorodheshwa wa kwanza Afrika. Hivi majuzi walishiriki kombe la dunia ila hatukuwa na bahati ya kufika huko Urusi.

Africa Cup 2019 | Senegal v Algerien
Senegal watazikosa huduma za beki wao Khalidou CoulibalyPicha: Getty Images/AFP/J. Soriano

Makala yaliyopita tulibanduliwa kwenye raundi ya kwanza kwa hiyo kwa sasa takwimu zote zinaelekea upande wa Senegal," alisema Belmadi.

Makocha wote hawa waliishi Ufaransa katika utoto wao na wote wana umri wa miaka 43. Walizichezea timu zao za taifa, Cisse akicheza kwenye fainali ya 2002 walipolazwa na Cameroon. Belmadi yeye aliichezea Algeria mara ishirini.

Wapo wanaoiweka karata yao kwa Algeria ila wapo pia wale wanaoamini kwamba Senegal watarudi Dakar na kombe hilo. Jawabu litabainika baada ya dakika tisini au mia moja na ishirini.