Netanyahu aapa kuendeleza mashambulizi dhidi ya Hezbollah
27 Septemba 2024Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo na kuapa kwamba nchi yake itaendelea na kampeni ya kijeshi dhidi ya kundi la Hezbollah hadi ifanikishe malengo iliyojiwekea kwenye mpaka na Lebanon.
Matamshi hayo ya Netanyahu yameondoa matumaini ya kupatikana makubaliano yatakayomaliza uhasama baina ya pande hizo mbili ambao unatishia kuzusha vita kamili kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.
Netanyahu amewaambia viongozi wa ulimwengu kwamba serikali yake haitavumilia tena mashambulizi ya maroketi ya kila siku yanayofyetuliwa na Hezbollah kwenye eneo hilo la mpaka.
Amesema watafanya kila linalowezekana kusambaratisha uwezo wa kijeshi wa Hezbollah ili kuwezesha raia wa Israel waliohamishwa kutoka mpaka na Lebanon wanarejea kwenye makaazi yao.
Kwa wiki siku kadhaa sasa jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi makali dhidi ya kile imekitaja kuwa ngome za kundi la Hezbollah nchini Lebanon, hujuma ambazo hadi sasa zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 600.