Israel yaapa kuendelea kupambana na Hezbollah hadi ushindi
26 Septemba 2024Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameyadhoofisha matumaini ya kupatikana kwa makubaliano na kundi la Hezbollah baada ya Marekani na washirika wengine kutoa wito wa kusimamisha mapigano kwa siku 21 ili kutoa nafasi kwa hatua za kidiplomasia.
Netanyahu amesema nchi yake itaendelea kupambana na wanamgambo wa Hezbollah hadi ipate ushindi kamili.
Katika taarifa iliyotolewa wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anaelekea mjini New York kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ofisi yake imesema kulikuwa na pendekezo tu, juu ya kusimamishwa mapigano na Waziri Mkuu hakuwa ametoa jibu la pendekezo hilo la kusimamisha mapigano kwenye mpaka wa kaskazini kati ya Israel na Lebanon.
Israel imesema inakaribisha hatua za kidiplomasia juu ya mgogoro wake na Lebanon, lakini haiko tayari kusitisha mapigano, mpaka malengo yake la kuisambaratisha Hezbollah yatakapotimia.
Soma Pia: Israel inapanga kuanzisha operesheni ya ardhini Lebanon
Taarifa hii imetolewa huku Israel ikitishia kuanzisha mashambulizi ya ardhini ndani ya Lebanon ili kuliondoa kundi la wanamgambo wa Hezbollah kutoka mpakani na baada ya Israel kufanya mashambulio ya anga katika kitongoji kimoja kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kuwaua watu 20 wengi wao kutoka Syria.
Jeshi la Israel pia limesema takriban makombora 45 yamerushwa kutoka Lebanon, na kuongeza kuwa baadhi yamezuiwa huku mengine yakitua katika maeneo yasiyo na watu.
Hezbollah imesema iliyaenga majengo ya idara ya ulinzi karibu na mji wa Haifa kaskazini mwa Israel.
Wingu zito la moshi lilionekana katika mji wa Beirut hii leo huku mlipuko mkubwa ukisikika katika viunga vya kusini mwa mji huo kulingana na mashahidi.
Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya anga mjini Beirut. Chanzo kimoja cha usalama kimeliambia shirika la Habari la Reuters kwamba Israel imemlenga kiongozi mkuu wa Hezbollah katika mashambulio yake kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut mchana wa leo, lakini hatma yake bado haijajulikana.
Soma Pia: Ulimwengu wataka Mashariki ya Kati isitumbukie vitani
Marekani, Ufaransa na washirika wengine wametoa tamko la pamoja la kutaka mapigano yasitishwe kwa siku 21, huku Rais Joe Biden, mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, na washirika wengine wakikutana kando ya mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa huko mjini New York.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebabon yamesababisha watu wapatao 90,000 kuhama makazi yao katika maeneo ambayo ni ngome za jadi za Hezbollah wakikimbilia kwenye maeneo salama kwingineko kwenye nchi hiyo ndogo iliyo kwenye Bahari ya Mediterania.
Vyanzo: AP/RTRE/AFP