1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege iliyombeba makamu wa rais wa Malawi imepoteza uelekeo

11 Juni 2024

Ndege ya kijeshi iliyokua imembeba makamu wa rais wa Malawi Saulos Chilima, sambamba na watu wengine tisa imepoteza uelekeo wake na kutojulikana ilipo.

https://p.dw.com/p/4gt7p
Saulos Chilima Malawi
Makamu wa Rais, Saulos Chilima, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makazi yake ya kibinafsi huko Lilongwe Februari 5, 2020.Picha: AMOS GUMULIRA/AFP

Taarifa kutoka ofisi ya rais imesema ndege hiyo ilianza safari yake majira ya saa tatu Asubuhi ya Jana kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Lilongwe, na ilipoteza mawasiliano kwenye maeneo ya milimani upande wa Kaskaziniwa nchi hiyo na kupelekea kushindwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu kama ilivyotarajiwa.

Akizungumza kwa njia ya televisheni Jumatatu jioni Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu alisema serikali inasubiri maelezo zaidi kuhusu tukio hilo kutoka kwa jeshi ambalo kwa sasa lipo katika jitihada za kuisaka ndege hiyo.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, amesitisha safari yake ya kikazi Bahamas

Kufuatia taarifa hiyo Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, amesitisha safari yake ya kikazi iliyokua imepangwa aelekee huko Bahamas, na ametoa maagizo kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo kuhakikisha wanafanya jitihada za kuitafuta ndege hiyo katika msitu wa Chikangawa.

Soma zaidi:Asilimia 44 ya mazao ya mahindi nchini Malawi yameathirika na ukame

Chilima amekuwa makamu wa rais tangu 2020. Alikuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Malawi wa 2019 na kushika nafasi ya tatu. Uchaguzi huo ulimalizika kwa kumpa ushindi mpinzaniwake Peter Mutharika lakini ulibatilishwa na Mahakama ya Katiba ya Malawi kwa sababu ya kasoro zilizojitokeza.