1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malawi yatangaza hali ya dharura kufuatia ukame

25 Machi 2024

Malawi imekuwa nchi ya pili baada ya Zambia kutangaza hali ya dharura kufuatia ukame ambao umezikumba wilaya 23 kati ya 28 za nchi hiyo. Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amesema nchi yake inahitaji msaada wa haraka

https://p.dw.com/p/4e5b0
Malawi
Malawi imetangaza hali ya dharura kufuatia ukame ambao umeathiri mazao nchini humoPicha: Mirriam Kaliza/DW

  
Malawi imekuwa nchi ya pili baada ya Zambia kutangaza hali ya dharura kufuatia ukame ambao umezikumba wilaya 23 kati ya 28 za nchi hiyo. Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amesema nchi yake inahitaji msaada wa haraka wa dola milioni 200 za kimarekani ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.

Soma zaidi. Wakulima wakabiliwa na ukame Kusini mwa Jangwa la Sahara

Malawi ndiyo nchi ya hivi karibuni katika ukanda wa nchi za kusini mwa Afrika kutangaza hali ya hatari kufuatia mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame na kupelekea kukauka kwa mazao.

Nchi jirani ya Zimbambwe pia imeshuhudia kukauka kwa mazao ya wakulima wake na iko mbioni kufuata nyayo za mataifa ya Zambia na Malawi kutangaza hali ya dharura kufuatia janga la ukame.

 Malawi
Mazao mengi hasa ya mahindi nchini Malawi yameharibika kutoka na ukame ulioikumba nchi hiyoPicha: Mirriam Kaliza/DW

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilielezea hofu yake juu ya kuzuka kwa ya hali hii inayoshuhudiwa katika mataifa haya ya kusini mwa Afrika na kwamba kungezuka njaa kutokana na athari za El Nino.

Mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa haraka

WFP ilisema kuwa tayari watu milioni 50 walikoko katika ukada wa mataifa ya kusini mwa Afrika wanakabiliwa na uhaba wa chakula kabla hata ya kutokea kwa ukame huu uaotajwa kuwa mkubwa zaidi kwa kipindi cha miaka kumi.

Huyu ni Brighton Mphinga, Afisa usimamizi wa masuala ya hatari katika wilaya ya Neno nchini  Malawi akiielezea hali ya chakula nchini humo.

“Chakula ulichoona tunasambaza leo ni cha msimu tuliopo, lakini kwa sasa kuna njaa nyingine  ambayo tunakabiliana nayo kwa sababu ya kiangazi tulichopata.wilaya ya Neno, imepigwa sana. Kwa hivyo, tamko la rais linamaanisha watu wengine watakuja zaidi, wakiomba msaada wa serikali mahali ambapo haikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Watu watakuja kwa sababu ya tamko hilo."

Soma zaidi. Malawi: "Tunawindwa kama wanyama"

Kwa upande mwingine, shirika la misaada la serikali ya Marekani, USAID,lilisema kuwa zaidi ya watu milioni 20 walioko kusini mwa Afrika wangehitaji msaada wa chakula haraka mapema 2024, kwa sehemu kutokana na athari ya El Niño.

WFP
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilielezea hofu ya kuzuka kwa njaa kwa mataifa ya kusini mwa Afrika kufuatia mvua za El NinoPicha: Privilege Musvanhiri/DW

Kwa mujibu wa wafuatiliaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani wa WFP, mwezi uliopita wa Februari ulikuwa ni mwezi mkavu na wa kiangazi zaidi katika miaka 40 kwa mataifa Zambia na Zimbabwe.

Mataifa mengine kama Malawi, Msumbiji na sehemu za Angola zilikuwa na upungufu mkubwa wa mvua na itakumbukwa kuwa mamilioni ya watu kusini mwa Afrika hutegemea chakula wanacholima ili kuishi.

Lazarus Chakwera: Tunahitaji msaada wa haraka

Kabla ya tangazo la hali ya hatari katika mataifa ya Malawi na Zambia, mashirika ya WFP na USAID tayari yalikuwa yamezindua mpango wa kulisha watu milioni 2.7 katika baadhi ya vijiji nchini Zimbabwe wanaokabiliwa na uhaba wa chakula.

Malawi / Lazarus Chakwera
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ameomba jumuiya ya kimataifa kuisadia Malawi msaada wa chakula katika kipindi hiki cha ukamePicha: AMOS GUMULIRA/AFP

Soma zaidi. Malawi yaanza zoezi la chanjo baada ya nchi hiyo kukumbwa na kimbunga

Shirika la misaada la Uingereza Oxfam lilisema mwezi huu kuwa zaidi ya watu milioni 6 nchini Zambia sawa na asilimia 30 ya wakazi wake  sasa wanakabiliwa uhaba wa chakula a utapiamlo.

Rais wa Malawi,  Lazarus Chakwera amesema kuwa amefanya ziara nchini mwake na kubaini kuwa karibu asilimia 44 ya mazao ya mahindi nchini Malawi yameathirika, watu milioni 20 wakiwa wanahitaji msaada wa haraka wa chakula wa tani 600,000 na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwapa msaada.