1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Umoja wa Ulaya zapokea chanjo za kwanza za Covid-19

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
26 Desemba 2020

Awamu ya kwanza ya chanjo ya virusi vya corona imewasili katika nchi zote za Jumuiya ya Ulaya leo Jumamosi, ikiwa ni siku moja kabla ya jumuiya hiyo kuanza rasmi mpango wa kutoa chanjo hiyo kesho Jumapili.

https://p.dw.com/p/3nErM
Deutschland Haar | Corona Impfstoff | Testung
Picha: picture-alliance/dpa/F. Hoemann

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema kwa hakika kupatikana kwa chanjo hiyo kwa wakati mmoja katika nchi za jumuiya ya Ulaya ni dhihirisho kuwa nchi hizo zimeshikamana pamoja. Watu wapatao milioni 450 wanaoishi katika nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya watapewa chanjo hiyo dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Von der Leyen amesema chanjo hiyo itaanza kutolewa katika miji ya Athens, Rome, Helsinki, Sofia na miji mingine. Amesema kuna matumaini makubwa kwamba chanjo hiyo itasaidia kurudisha maisha ya kawaida. Wakati huo huo rais huyo wa Tume ya Ulaya amewahimiza watu kuweka tahadhari kwa ajili ya kuzuia kuenea zaidi kwa janga hilo.

Soma zaidi: Pfizer na BioNTech: Chanjo ya Covid-19 ina ufanisi wa 90%

Umoja wa Ulaya umeidhinisha chanjo iliyotengenezwa kwa pamoja na kampuni za BioNTech na Pfizer ambayo majaribio yake yameonyesha kuwa na ufanisi wa asilimia 95 katika kuzuia virusi vya Corona. Chanjo hiyo tayari iliishaanza kutumika katika nchi za Uingereza, Marekani na Canada.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Olivier Hoslet/REUTERS

Huko Malta, nchi ndogo zaidi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Waziri Mkuu Robert Abela amesema usafirishaji wa dozi za chanjo umeleta matumaini katika nchi hiyo ya visiwani. Abela amesema njia ya kurudi katika hali ya kawaida katika maisha ya watu wake imeanza leo Jumamosi.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn ametoa wito wa kufanyika juhudi kubwa za kitaifa ili kuwapa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 watu wengi iwezekanavyo. Zoezi la utoaji wa chanjo hiyo limepangiwa kuanza kesho Jumapili. Spahn amesema chanjo hiyo ni muhimu katika kupambana na janga la virusi vya Corona.

Angalia: 

Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 zitaanza kutolewa kuanzia kesho hapa Ujerumani. Dozi za kwanza tayari zimewasilishwa katika majimbo yote 16 ya Ujerumani leo Jumamosi. Watu wenye umri wa zaidi ya miaka 80 na wahudumu wa afya watakuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo. Spahn amesema siku ya Jumapili tarehe 27.12.2020 itakuwa ni siku muhimu katika historia ya Ujerumani na amesisitiza kuwa nchi hiyo imejiandaa vizuri.

Spahn amesema nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitaendelea kushirikiana pamoja katika mgogoro huu wa janga la corona na ametoa wito kwa vijana kuonyesha mshikamano na wazee na watu wengine dhaifu, ambao ndio wanahitaji kupewa kipaumbele katika kupewa chanjo.

Vyanzo:DPA/AP