Nchi za magharibi zakosoa kuahirishwa uchaguzi Sudan Kusini
21 Septemba 2024Mataifa matatu ya magharibi leo yameelezea wasiwasi wao mkubwa kufuatia tangazo la kuahirishwa kwa miaka miwili uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini Sudan Kusini.
Marekani, Uingereza na Norway zimesema kwa pamoja kwamba uamuzi huo wa kurefusha utawala wa kipindi cha mpito nchini Sudan Kusini ni ishara ya kushindwa viongozi wa taifa hilo kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa amani.
Soma zaidi. Sudan Kusini yaahirisha uchaguzi wa Desemba kwa miaka miwili
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011 lakini miaka miwili baadaye ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo inakadiriwa vimewaua zaidi ya watu 400,000. Wiki iliyopita ofisi ya Rais Salva Kiir ilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba mwa huu ambao ungekuwa wa kwanza tangu uhuru.
Uchaguzi huo ulikuwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha utulivu kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo uhasama kati ya wanasiasa wawili vigogo, Rais Kiir na mpinzani wake Riek Machar umesababisha taathira za kutisha kwenye ustawi wake.