Umoja wa Mataifa kuwawekea vikwazo makamanda wa RSF Sudan
28 Agosti 2024Marekani imependekeza rasmi kuwawekea marufuku ya kusafiri na kuzuiwa kwa mali zao mkuu wa oparesheni wa RSF Osman Mohamed Hamid na kamanda wa RSF magharibi mwa Darfur AbdelRahman Juma Barkalla.
Iwapo wawili hao watafanikiwa kuwekewa vikwazo, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan na ambavyo vilizuka katikati ya mwezi Aprili mwaka uliopita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha RSF.
Soma pia: Marekani kuanzisha mazungumzo ya amani ya Sudan, licha ya jeshi kutothibitisha
Kamati ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yenye wanachama 15 hufanya kazi kwa muundo wa maafikiano. Iwapo hakuna mtu atakayepinga pendekezo hilo la kuwekewa vikwazo makamanda hao wawili wa RSF kufikia Ijumaa mchana, basi moja kwa moja vikwazo hivyo vitatekelezwa.
Wanachama pia wanaweza kuomba muda zaidi wa kuzingatia pendekezo hilo, kuliweka katika hali ya kusubiri au kulipinga kabisa.