1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Nawaz Sharif kuwania uchaguzi ujao Pakistan

Saleh Mwanamilongo
28 Desemba 2023

Tume ya uchaguzi nchini Pakistan leo imeridhia uteuzi wa waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif kuwania uchaguzi ujao wa Februari mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/4aflD
Nawaz Sharif waziri mkuu wa zamani wa Pakistana nayetaka kuwania muhula wa nne
Nawaz Sharif waziri mkuu wa zamani wa Pakistana nayetaka kuwania muhula wa nnePicha: Ali Kaifee/DW

Hata hivyo Nawaz Sharif bado anahitaji kuondolewa marufuku ya kushiriki uongozi wa umma ili kukidhi vigezo vya kuwania nafasi yoyote na hivyo haijawekwa wazi mchakato wa kuteuliwa kwake. Mahakama inatarajiwa kusikiliza shauri dhidi ya marufuku hiyo mnamo mwezi Januari.

Sharif alipigwa marufuku kushiriki uchaguzi na Mahakama ya Juu manamo 2017 ambayo ilimtangaza kuwa si mwaminifu kwa kutofichua mapato kwenye kampuni inayomilikiwa na mwanawe.

Changamoto kubwa kwa Nawaz Sharif ni kurejesha uungwaji mkono kutoka kwa mpinzani wake wa karibu ambae ni nyota wa zamani wa kriketi Imran Khan, ambae pia licha ya kuwa gerezani kwa shutuma za ufisadi ni maarufu kwenye siasa za Pakistan baada kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri Mkuu mnamo 2022. Khan mwenye umri wa miaka 71, ameondolewa kwenye uchaguzi kwa kukutwa na hatia ya ufisadi, ambayo ameikatia rufaa. Imran Khan pia aliwasilisha uteuzi wa uchaguzi ujao hapo Ijumaa.

Wananchi wakosa imani kwa wanasiasa

Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan mpinzani wa Sharif yuko jela kwa tuhuma za rushwa
Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan mpinzani wa Sharif yuko jela kwa tuhuma za rushwaPicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Sheria za Pakistan zinakataza mtu aliyetiwa hatiani kugombea kiti cha ubunge na kuzuia matarajio yake ya kuwa waziri mkuu. Nawaz Sharif, ambaye alirejea nyumbani Oktoba kutoka miaka minne ya uhamisho alimojipeleka mwenyewe huko London, Uingereza anatarajiwa kuwania muhula wa nne wa uwaziri mkuu katika uchaguzi wa tarehe 8 Februari. Wachambuzi wamesema uhusiano wa Sharif na jeshi lenye nguvu la Pakistan, ambalo huamua zaidi nani atatawala taifa hilo la watu milioni 241, sasa uko katika hatua nzuri ambayo inaweza kumuinua dhidi ya wapinzani wake.

Kupanda kwa bei ya maisha 

Pakistan inapitia changamoto ya usalama, kudorora kwa uchumi wa taifa hilo na mgogoro wa kisiasa wakati ikijitayarisha kufanya uchaguzi huo mkuu. Mfumuko wa bei wa Pakistan ulipanda hadi rekodi ya asilimia 31.4 mwezi Septemba, ambapo bei za nishati zimekuwa juu hasa.

Kutokuaminiana kati ya taasisi za serikali ni kukubwa sana kiasi kwamba uchaguzi ujao hauhusu tena ni chama gani kitashinda viti vingi katika bunge lijalo; ni kuhusu kunusurika kwa Pakistani kama taifa la kisasa, watu wengi wanasema.

Wataalamu wanaamini kuwa idadi ya wapiga kura itakuwa ndogo pengine zaidi katika historia ya uchaguzi nchini Pakistan.