Pakistan yamruhusu Sharif kurejea nyumbani kutoka uhamishoni
20 Oktoba 2023Mahakama ya Pakistan imetoa dhamana ya ulinzi kwa waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif na kumruhusu kurejea nyumbani kutoka uhamishoni. Wakili anayemtetea amesema dhamana hiyo ya ulinzi inazuia mamlaka kumkamata Sharif hadi atakapofikishwa mahakamani Oktoba 24. Waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan anatarajiwa kurejea nchini humo siku ya Jumamosi.
Sharif alitimuliwa kwa ufisadi mwaka 1993, na kurejea tena katika wadhifa huo mwaka 1997. Lakini aling'olewa miaka miwili baadaye katika mapinduzi ya kijeshi. Mahakama ya juu ilimpiga marufuku kushiriki siasa maisha yake yote kutokana na tuhuma za ufisadi, ambazo anazikanusha. Mwaka 2018, alipatikana na hatia kwa makosa ya ufisadi na akahukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani. Lakini mnamo mwaka 2019, mahakama ilimruhusu kusafiri kwenda London kwa matibabu na kuamua kubaki uhamishoni.