1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Napoli wakaribia taji la kwanza tangu enzi za Maradona

24 Aprili 2023

Napoli wanakaribia kulibebea taji la Serie A nchini Italia baada ya kuwalaza Juventus 1-0 katika mechi iliyochezwa Jumapili.

https://p.dw.com/p/4QUFA
Fußball Champions League | SSC Neapel - AC Mailand
Picha: Maurizio Borsari/AFLOSPORT/IMAGO

Bao la pekee katika mechi hiyo lilifungwa na mshambuliaji Giacomo Raspadori kunako dakika za mwisho za mechi.

Ushindi huu umewapelekea Napoli ambao wako chini ya ukufunzi wa Luciano Spaletti, kukaribia kusherehekea taji lao la kwanza la Serie A tangu enzi za Diego Maradona alipokuwa mchezaji wa klabu hiyo.

Huenda wakatawazwa ubingwa hata mwishoni mwa wiki hii iwapo wataifunga Salernitana nyumbani na Lazio walio kwenye nafasi ya pili washindwe kuifunga Intermilan.

Kwengineko kocha wa Juventus Massimiliano Allgeri baada ya mechi ya Jumapili amesema wanachokilenga kwa sasa ni kumaliza msimu katika nafasi ya pili.

Fußball Europa League | SC Freiburg vs Juventus Turin
Wachezaji wa Juventus wakisherehekea kufunga goliPicha: Nderim Kaceli/LiveMedia/Independent Photo Agency/IMAGO

Hao Bianconeri mwishoni mwa wiki iliyopita walirudishiwa pointi 15 walizokuwa wamepokonywa na shirikisho la kandanda nchini humo kutokana na kutoeleweka kwa mahesabu ya fedha klabuni humo na sasa wako miongoni mwa timu nne bora tena.

Na sasa Allegri anasema kupokonywa pointi hizo kuliwaathiri wachezaji wake.

"Ni wazi kwamba ilituathiri ila hatustahili kutafuta kisingizio. Kilichofanyika kimefanyika, sasa tunachostahili kufanya ni kupata matokeo mazuri kuanzia sasa hadi Juni 4," alisema Allegri.