Naibu Rais wa Kenya 'anaumwa sana' mawakili wake wasema
17 Oktoba 2024Mawakili wanayemuwakilisha Naibu wa Rais nchini Kenya Rigathi Gachagua katika kesi ya kuondolewa kwake madarakani wameondoka katika bunge la seneti huku vikao vikiendelea baada ya bunge hilo kuamua kuendelea na vikao hivyo bila uwepo wa mteja wao, Gachagua.
Wakili mkuu wa naibu huyo wa rais alikuwa ameliambia bunge hilo kuwa Gachagua "anaumwa sana" na amelazwa hospitali.
Wakili Paul Muite amesema kwamba Gachagua ana maumivu makali ya kifua.
Hii ni baada ya Naibu huyo wa rais kushindwa kurudi katika bunge hilo kutoa ushahidi kama ilivyokuwa imeratibiwa.
Gachagua aliyekuwa bungeni katika kikao cha asubuhi alikuwa anatarajiwa kujitetea kwenye kikao cha mchana kuhusu madai 11 yaliyowasilishwa mbele ya Baraza la Seneti siku ya Alhamisi, kabla maseneta kupiga kura ya kumuondoa madarakani baadae Alhamisi.