Mzozo wa Urusi na Ukraine watimiza mwezi mmoja
24 Machi 2022Takriban watu wanne wameuawa, wakiwemo watoto wawili, na wengine sita wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya jana usiku mashariki mwa Ukraine. Gavana wa eneo la Lugansk, Sergiy Gayday amevishutumu vikosi vya Urusi kwa kutumia silaha nzito katika kijiji cha Rubizhne.Viongozi wa NATO, G7 na EU kujadili uvamizi wa Urusi
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema serikali ya Urusi haina nia ya kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Ukraine kwa sasa, kwani Moscow haijafikia kile inachotaka katika uvamizi wake. Borell amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya na washirika wake wataendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa jeshi la Ukraine.
Akizungumza kabla ya mkutano wa kilele wa Jumuia ya Kujihami ya NATO unaofanyika leo mjini Brussels nchini Ubelgiji, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema Rais Putin amefanya kosa kubwa la kuanzisha vita dhidi ya taifa lililo huru na kwamba amepuuza nguvu za jeshi na ushujaa wa watu wa Ukraine. Stoltenberg amesema viongozi wa NATO katika mkutano huo watajidili ni jinsi gani wataendelea kuisaidia Ukraine.
Urusi yabadili mfumo wa mashambulizi yake
Shirika la habari la Associated Press limemnukuu afisa mkuu wa ulinzi wa Marekani akisema kuwa vikosi vya Urusi havijaribu tena kusonga mbele kuelekea Kyiv, na kwamba wanajeshi wa Urusi sasa wanazidisha shinikizo katika maeneo ya mashariki ya Luhansk na Donetsk.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ametaka raia wa dunia nzima kuandamana kwa ajili ya amani dhidi ya uvamizi huo wa Urusi na kusema wataendelea kuzungumza.
"Tunauangalia uhalisia, tutaendelea kuzungumza na kuhimiza mazungumzo hadi tutakapopata njia itakayotuwezesha kuliambia taifa letu hivi ndivyo tutakavyolinda amani. Amani. Ni lazima tufahamu kwamba kila siku ya mapigano, kila siku ya upinzani, hututengenezea hali bora zaidi, hufanya msimamo wetu kuwa na nguvu zaidi ili kuhakikisha mustakabali wetu duniani."
Mkuu wa idara ya ujasusi na ulinzi nchini Uingereza Jim Hockenhull amesema Urusi sasa inaendesha vita vya "uhasama" nchini Ukraine baada ya Moscow kushindwa kufikia malengo yake ya awali huku akionya kwamba vita vya uhasama vitahusisha matumizi ya silaha kiholela na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu ya Ukraine kuongezeka na hivyo kuuzidisha mzozo wa kibinadamu.
Vyanzo: AFPE,DW