1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aitisha maandamano duniani kote kuipinga Urusi

24 Machi 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito kwa watu duniani kote kuandamana barabarani kama hatua ya kupinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/48xSL
BG | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Patrick Doyle/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelihutubia bunge la Ufaransa na kutumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za Ufaransa ambazo bado zinaendesha oparesheni zake nchini Urusi, "kuacha kufadhili" hujuma inayofanywa na Urusi kwa Ukraine. Katika ujumbe wake wa dakika 15, Zelensky aliyevaa fulana ya rangi ya kijani kibichi ameonekana kuwasuta watu wanaofaidika kifedha na vita hivyo.

Rais huyo wa Ukraine hasa alizitaja kampuni ya magari ya Ufaransa ya Renault, Auchan na kampuni ya mapambo ya nyumba na fanicha ya Leroy Merlin akizitaka kuacha kuifadhili Urusi inayotumia fedha hizo kumwaga damu za watu wa Ukraine.

Soma zaidi: Ukraine yasema jeshi lake laendelea kusimama imara kuilinda nchi

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, alikwenda mbali zaidi kwa kutoa wito wa kususiwa kwa kampuni kongwe ya Renault, inayosifika barani Ulaya kwa utengenezaji wa magari. Wabunge wa Ufaransa waliipongeza hotuba ya Zelenksy, ambaye amekuwa akizungumza na mabunge mbalimbali ya Ulaya ili kutafuta uungwaji mkono.

Wito watolewa wa kususia kampuni ya magari ya Ufaransa ya Renault

Russland I Renault-Autowerk in Moskau
Kampuni ya magari ya Ufaransa Renault inayohudumu nchini UrusiPicha: Stanislav Krasilnikov/TASS/picture alliance

Uwepo wa zaidi ya kampuni 500 za Ufaransa nchini Urusi kumezua mjadala mpana nchini Ufaransa, katikati ya shinikizo ya kuzitaka kampuni hizo zijiunge na kampuni nyengine za Marekani na Uingereza kukata uhusiano na Moscow. Tayari kampuni za McDonald, Apple na BP zimesitisha oparesheni zake nchini Urusi. Hata hivyo, hakuna kampuni yoyote ya Ufaransa iliyofunga matawi yake nchini Urusi.

Katika ujumbe alioutoa kuelekea mkesha wa kumbukumbu ya mwezi mmoja wa uvamizi wa Urusi, Zelensky amewataka watu duniani kote kusimama imara dhidi ya Urusi na kupinga vita hivyo. Rais huyo wa Ukraine pia ametoa wito kwa muungano wa jeshi la kujihami la NATO kuipa msaada Ukraine ikiwemo wa silaha ili kupambana na wanajeshi wa Urusi. 

Biden amewasili Brussels kwa mkutano wa kujadili vita vya Ukraine

Joe Biden zum Gesetz gegen Gewalt an Frauen
Rais wa Marekani Joe Biden amewasili mjini Brussels kwa mkutano wa EU na NATOPicha: Tom Brenner/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden amewasili barani Ulaya kwa ajili ya mkutano na washirika wake wa Magharibi ili kujadili juu ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

Akizungumzia juu ya jinsi mzozo nchini Ukraine unavyozidi kuwa mbaya, Biden amewaambia waandishi habari wakati akipanda ndege katika Ikulu ya White House kuelekea Ulaya kwamba, anaona tishio la wazi la Urusi kutumia silaha za kemikali katika vita vya Ukraine.

Soma pia:Baadhi ya Warusi wataka kuukana uraia wao

Ikitokea iwapo wanajeshi wa Urusi watapoteza nguvu, basi upo uwezekano kwamba Rais Vladimir Putin anaweza kuamuru mashambulizi ya silaha za kemikali. Hali hiyo ni mojawapo ya ajenda ya mkutano wa mataifa yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani G7, NATO na Umoja wa Ulaya mjini Brussels leo Alhamisi.

Biden anatazamiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya NATO hii leo alafu kesho Ijumaa atasafiri kwenda Poland- jirani wa Ukraine na ambayo imewapa hifadhi zaidi ya wakimbizi wa Ukraine milioni 3.6.Mnamo siku ya Jumamosi atakutana na Rais Andrzej Duda kabla ya kurudi Washington.

Wakati hayo yanaarifiwa, Ukraine ambayo bado inapambana kufa kupona, imetoa wito kwa muungano wa jeshi la kujihami la NATO kuipa silaha zaidi ili kupambana na wanajeshi wa Urusi.

Soma pia:Rais Joe Biden amwita Putin kuwa mhalifu wa kivita 

Meya wa mji wa Kyiv, bingwa wa zamani wa mchezo wa ndondi duniani Vitali Klitschko amesema wanajeshi wa Ukraine kwa ujasiri mkubwa wanapambana na wanajeshi wa Urusi na wamefanikiwa kwa kiasi fulani kuwarudisha nyuma katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu.

Afisa mwandamizi wa NATO amewaambia waandishi wa habari kuwa, wanajeshi 15,000 wa Urusi huenda ikawa wameuawa katika vita hivyo japo licha ya mafanikio hayo, mshauri mkuu wa Zelensky Andriy Yermak amesema bado Ukraine inahitaji msaada zaidi.