1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia ataka Ukatibu Mkuu NATO

28 Novemba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia ametangaza nia ya kuwania Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO, akisema muungano huo wa kijeshi unahitaji mtu anaejenga muafaka na mwenye maono ya wazi juu ya kuishughulikia Urusi.

https://p.dw.com/p/4ZXhg
Latvia I Waziri wa Mambo ya Nje I Krisjanis Karins
Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia Krisjanis Karins anataka kuwa Katibu Mkuu wa NATO.Picha: Olivier Matthys/AP/dpa/picture alliance

NATO huenda ikamteua katibu mkuu mpya wakati wa mkutano wake ujao wa kilele mjini Washington mnamo mwezi Julai mwaka ujao. Waziri Mkuu wa zamani wa Norway Jens Stoltenberg amekuwa raia wa juu wa muungano huo tangu 2014. Muhula wake umerefushwa mara nne wakati wa vita vya Ukraine.

"Tunaelekea kuwa na mataifa 32. Kuyaweka mataifa 32 pamoja kuhusu mada yoyote, ni changamoto kubwa, na tunahitaji kiongozi anaeweza kujenga muafaka na anaeweza kufanya kazi na mshirika yeyote na wote, kumpeleka mbele kila mmoja katika mwelekeo sawa," waziri wa mambo ya nje wa Latvia Krisjanis Karins aliwaambia waandishi habari katika makao makuu ya NATO.

Moja ya changamoto za Stoltenberg ni kuishawishi Uturuki, pamoja na Hungary, kuidhinisha maombi ya Sweden kuwa mwanachama wa 32 wa NATO. Maafisa wa NATO wanatumai suala hilo litatatuliwa kufikia wakati Rais Joe Biden na washirika watakapokutana mjini Washington.

Karins alikuwa waziri mkuu wa Latvia kwa karibu miaka mitano - NATO hupendelea makativu wakuu ambao wamehudumu katika nafasi za juu serikalini - na alisimamia ongezeko la matumizi ya kijeshi. Alisema nchi yake itatumia asilimia 2.4 ya pato jumla la ndani mwaka huu, kiwango ambacho ni cha juu kuliko lengo la jumuiya hiyo la asilimia 2.

Latvia - Krisjanis Karins
Krisjanis Karins anasema NATO inahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kujenga muafaka na mwenye maono ya wazi kuhusu namna ya kuishughulikia Urusi.Picha: Gints Ivuskans/AFP/Getty Images

Urusi inasalia kuwa hasimu wa kihistoria wa NATO, na kusimamia mkakati wa muungano huo kuelekea Moscow ni mtihani mkubwa. "Katibu Mkuu ajaye anapaswa kuwa na maono ya wazi kuhusu mustakabali wa NATO, namna itakavyopanuka, namna itakavyofanya kuidhibiti Urusi," alisema Karins.

Soma pia:Uturuki yakubali kuiunga mkono Sweden kujiunga NATO 

Alisema ni muhimu kutoweweseka huku akikiri "kitisho halisi cha Urusi" na kuahidi kufanya kazi kukishughulikia. "Inawezekana," alisema. "Tunaweza kufanya hivyo tukiwa watulivu lakini wenye dhamiri.

Wakati Urusi ikishughulishwa na vita vyake nchini Ukraine, mchakato wa kumtafuta katibu mkuu mpya umekuwa wa kisiasa zaidi. Estonia, Latvia, Lithuania na Poland zimechukuwa msimamo usiyotetereka katika kuiunga mkono Ukraine, na hili linaweza kuifanya kuwa vigumu kwa mmoja wa viongozi wao kupata nafasi hiyo ya juu.

Muungano wa muafaka

Mataifa mengi ya NATO yanapendelea kumchagua mwanamke katika nafasi hiyo. Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas anazingatiwa kuwa mgombea mwenye nafasi imara. Waziri Mkuu wa Denmark Matte Frederiksen alizingatiwa kuwa mwenye nafasi kubwa baada ya kukutana na Biden katika majira ya kiangazi, lakini baadae alisema hatowania.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameondoa uwezekano wa yeye kuwania nafasi hiyo pia. Waziri Mkuu anaeondoka Uholanzi Mark Rutte ni mgombea anaepewa nafasi kubwa pia.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa sasa wa NATO Jens Stoltenberg amerefushiwa muhula wake mara nne kutokana na vita nchini Ukraine.Picha: Petr Stojanovski/DW

Makatibu wakuu wa NATO wanachaguliwa kwa muafaka. Hakuna mchakato rasmi wa kuwateuwa, na wanadiplomasia wamesema hakuna mchujo rasmi unafanyika kwa sasa.

Raia wa juu wa shirika hilo anahusika na kuongoza mikutano na kuelekeza baadhi ya wakati, mashauriano kati ya mataifa wanachama kuhakikisha kwamba miafaka inapatikana ili muungano unaofanyakazi kwa muafaka uendelee kufanya kazi.

Soma pia: Nini kitatokea iwapo Ukraine itajiunga na NATO?

Katibu Mkuu pia anahakikisha kwamba maamuzi yanatekelezwa, anazungumza kwa niaba ya mataifa yote kwa sauti moja, na ni nadra kwake kumkosoa mwanachama yeyote.

Stoltenberg ameweza kutekeleza hayo, akijizuwia kuwakosoa wanachama wanaoongozwa na marais na mawaziri wakuu wanaochukuwa hatua kivyao kama Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan au Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban.