1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswada wa Marekebisho Vyama vya Siasa Kenya kujadiliwa 2022

Shisia Wasilwa
30 Desemba 2021

Kiongozi wa wengi bungeni nchini Kenya, Amos Kimunya amemwandikia barua Spika kuomba kifanyike kikao maalum tarehe 5 hadi 7 mwezi Januari ili kuukamilisha mjadala wa vipengele ambavyo havikupigiwa kura.

https://p.dw.com/p/44zOj
Kenia Parlament Austritt Römisches Statut
Picha: Simon Maina/AFP via Getty Images

Barua hiyo ameiandika kutokana na wabunge hao kuamua kuvua uheshimiwa wao na kuligeuza Bunge la Kenya kuwa ukumbi wa masumbwi na cheche za maneno makali siku ya Jumatano, walipokuwa wakijadili muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa uliojadiliwa hadi usiku wa manane bungeni. 

Kupitia muswada huo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walilenga kubadilisha sheria ya vyamakujiunga kwenye muungano wa siasa bila ya kupoteza utambulisho wao. Na kikao maalum cha bunge hilo hadi kilipositishwa Jumatano usiku wa manane, ni marekebisho manne kati ya 23 ya muswada huo yaliyokuwa yamepigiwa debe.

Wabunge 150 wa upande wa Rais Kenyatta na Raila wakiunga mkono muswada huo dhidi ya 118 wa upande wa Ruto, hivyo kuonyesha ubabe wa kisiasa wa washirika hao wa salama za heri. Kiongozi wa wengi bungeni Amos Kimunya amemuandika spika waraka akitaka kikao hicho kirejewe mwakani ili marekebisho yaliyosalia yahitimishwe.

Kenia Präsident Uhuru Kenyatta und Oppositionsführer Raila Odinga in Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila OdingaPicha: Reuters/T. Mukoya

Hata hivyo zogo na vurugu vilitawala kipindi kirefu cha mdahalo huo, huku Mbunge wa Sigowet-Soin Kipsengeret Koros akijeruhiwa usoni kwenye vurugu hizo. "Mheshimiwa Spika…Hatuwezi kukubali kujeruhiwa bungeni. Hili haliwezi kufanyika mheshimiwa Spika," alisema Koros.

Kura ya muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa ulicheleweshwa, licha ya shughuli hiyo kuendelea hadi usiku wa manane, huku washirika wa makamu wa Rais William Ruto, wakilaumiwa kwa kutumia mbinu chafu kufanikisha hilo. Baadhi ya wabunge hao walianza kupiga kelele kwa umoja wakijitapa kuwa chama UDA kilikuwa maarufu kote nchini Kenya.

Spika asitisha kikao

Kwa wakati mmoja Spika wa Bunge alilazimika kusitisha kikao hicho kila baada ya muda fulani vurugu zilipozidi. Ruto anashikilia kuwa mswada huo una malengo fiche yanayonuia kufaidi Muungano wa Azimio la Umoja utakaotumiwa Raila kwenye uchaguzi mkuu ujao.  

Muswada huo unaelezea utaratibu unaostahili kuzingatiwa wa kusajili muungano wa vyama vya siasa pamoja na mwafaka baina ya washirika. Aidha mswada huo unaeleza kuwa chama cha Muungano hakitakiwi kuwa na ushirika na muungano mwingine. Wachambuzi wa siasa wanashikilia kuwa, mswada huo ni moja ya mkakati ambao kiongozi wa ODM Raila Odinga anapanga kutumia kwenye azma yake ya kuelekea ikulu. 

Wabunge kadhaa waliingia katika eneo la Spika huketi na kuanza kurushiana nmakonde, huku wengine wakirusha chupa za maji.. Kiongozi wa wachache John Mbadi alitimuliwa bungeni kwa siku tano kwa vurugu hizo zilizosababisha kujeruhiwa kwa mbunge huyo wa Sigowet. Taswira ya bunge hiyo jana ikichora mvutano unaotarajiwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu mwakani.