Museveni atimiza miaka 38 madarakani akililia ufisadi
26 Januari 2024Alipoingia madarakani mwaka 1986 kwa mtutu wa bunduki, Museveni alitoa ahadi kadhaa akielezea kuwa uongozi wake ungelilenga kukomesha maovu ambayo viongozi waliomtangulia waliyafanya na kuitumbukiza Uganda katika kipindi kirefu cha msukosuko wa kisiasa na kiuchumi.
Kwa namna hii aliwashawishi Waganda wengi kumuamini na wanampongeza kwa juhudi kadhaa za kunyanyua uchumi wa nchi ijapokuwa ametegemea zaidi wawekezaji wa kigeni kuleta mtaji.
Soma zaidi: Wapinzani Uganda waungana kumkabili Museveni 2026
Hii, kwa mtazamo wa wadadisi, imewawezesha wageni kuudhibiti uchumi kuanzia sekta ya viwanda, benki na mawasiliano.
Kwa upande wake, Rais Museveni amesisitiza kuwa mapungufu makubwa katika kujenga uchumi wa kizalendo ni kutokana na baadhi ya wapinzani kuichafulia Uganda sifa katika mataifa ya kigeni na kuwatia mashaka wawekezaji kutoka mataifa hayo kusita kuwekeza katika miradi muhimu kama vile ile ya mafuta na gesi.
Aidha amekosoa ufisadi na mifumo ya urasimu miongoni mwa watumishi wa serikali na taasisi za umma, lakini akaelezea kuwa anazidi kupata suluhu kwa vizingiti hivyo.
"Kuondoa urasimu katika serikali hasa katika mchakato wa zabuni na utoaji kandarasi ili kuwavutia wawekezaji wapya na kuzidisha vita dhidi ya ufisadi ndiyo mikakati ambayo tunazingatia na kwa hiyo ifahamike kuwa vita dhidi ya ufisadi si vigumu kama watu wanavyofikiria." Alisema Museveni.
Wadadisi mbalimbali wamelezea kuwa udhaifu wa utawala wa Museveni katika miaka 38 ya utawala wake ni kutokuwa na msimamo thabiti wa kupambana na ufisadi.
Ufisadi kuwa jambo la kawaida
Hali hii imesababisha maovu hayo kuwa ya kawaida ikiwemo kuwepo kwa upendeleo katika utoaji fursa za kazi, kandarasi na miradi.
"Ufisadi ni wazi, neno hilo linatumika kufunika wizi ambapo watu wananyakua mali za umma waziwazi, na unamuuliza jenerali museveni ana dawa aina gani akiwa ana hofia kila mara kuwadhibu watu wanaoiba raslimali za Waganda." Alisema Wambete Wamoto, mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Soma zaidi: Museveni aapa kuwaandama waliouwa watalii, muongozaji wageni
Katika hotuba yake ya mkesha wa siku hii ya ukombozi na pia kwenye sherehe za kitaifa, Museveni amekariri kuwa Uganda itapata mafanikio makubwa kiuchumi katika kipindi cha miaka kumi ijayo ambapo pato jumla la taifa litakuwa kwa asilimia 100 kutokana na sekta ya mafuta na pia kuimarishwa kwa raslimali watu kutokana na elimu na mafunzo yanayozingatia teknolojia za kisasa kama vile akili bandia..
Sherehe za kitaifa zimefanyika mji mkuu wa Jinja eneo la Busoga ambako Rais Museveni ameahidi kuongoza katika kupambana na hali ya umasikini na huduma duni kanda hiyo.