Mshindi wa tuzo ya Nobel ahukumiwa miaka 10 jela Belarus
3 Machi 2023Bialiatski na wanaharakati watatu wengine wakuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Viasna, wamepatikana na hatia ya kufadhili vitendo vya kuvuruga utulivu wa umma na magendo.
Valiantsin Stefanovich alipewa hukumu ya kifungo cha miaka tisa jela, Uladzimir Labkovicz miaka saba na Dzmitry Salauyou akahukumiwa kifungo cha miaka nane jela, licha ya kutokuwepo mahakamani.
Soma pia: Lukashenko: Tunaiunga mkono China kuhusu Ukraine
Bialitski na washirika wake wawili walikamatwa na kufungwa gerezani kufuatia maandamano makubwa ya umma juu ya uchaguzi wa mwaka 2020, uliompa nafasi kiongozi wa kiimla Alexander Lukashenko kuingia madarakani kwa muhula mwengine.
Salauyou alifanikiwa kuikimbia Belarus kabla ya kukamatwa.
Bialitski alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2022
Mwaka jana, alipokuwa gerezani akisubiri kesi dhidi yake ianze, Bialitski alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel, pamoja na Wakfu mmoja wa Urusi wa kutetea uhuru wa raia na shirika la haki za binadamu la Ukraine.
Lukashenko ambaye ameitawala Belarus, nchi ya zamani ya uliokuwa muungano wa Kisovieti kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1994, alianzisha kamata kamata ili kuzima maandamano hayo, ambayo yalikuwa makubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo. Zaidi ya watu 35,000 walikamatwa, na maelfu ya wengine walishambuliwa na polisi.
Soma pia: Belarus yafungua mashtaka dhidi ya kiongozi wa upinzani
Wakati wa vikao vya kesi hiyo, iliyofanyika kwa usiri mkubwa, Ales Bialiatski mwenye umri wa miaka 60 pamoja na wanaharakati wenzake walikuwa wamefungiwa ndani ya chumba kimoja katika mahakama. Wanaharakati hao wamekaa kizuizini kwa muda wa miezi 21 tangu walipokamatwa.
Katika picha zilizopigwa ndani ya mahakama na ambazo zimetolewa leo Ijumaa na shirika la habari la serikali-Belta, wanne hao walionekana wachovu japo watulivu huku wakiwa wamevaa nguo nyeusi.
UN yakosoa hukumu ya mahakama ya Belarus
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Ravina Shamdasani amesema, "Tumesikitishwa sana na kesi ya wanaharakati hawa wa haki za binadamu wa Belarus. Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu ukosefu wa haki na uhuru wa mahakama nchini Belarus, na kuwaweka watetezi wa haki za binadamu katika hatari ya kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa kazi yao halali ya kutetea haki za binadamu. Ninafahamu kuwa kufikia mwisho wa mwaka 2022, kulikuwa na watu wasiopungua 1,446, wakiwemo watoto 10, waliokuwa wakishikiliwa, na kukabiliwa na kesi.”
Shirika la kutetea haki za binadamu la Viasna limesema kuwa, licha ya hukumu hiyo kutolewa dhidi yao, wanaharakati hao wamekanusha kuhusika na vitendo vya kuvuruga utulivu wa umma na magendo.
Soma pia:Mazungumzo ya Urusi, Ukraine yapiga hatua kidogo
Katika hotuba yake ya mwisho mahakamani, mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel alitoa wito kwa mamlaka kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Ameeleza kuwa, ni dhahiri kwamba wachunguzi waliokuwa wakifuatilia kesi yake wametimiza jukumu walilopewa nalo ni: "kuwanyima uhuru kwa gharama zozote wanaharakati wa shirika la kutetea haki za binadamu la Viasna, kulitokomeza shirika hilo na kusimamisha kazi zao."
Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliyeko uhamishono Sviatlana Tsikhanouskaya ameshtumu uamuzi wa mahakama na kuuita "wa kutisha." Ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba, "Ni lazima tufanye kila linalowezekana kupambana na dhulma hii ya aibu na kuwaweka huru."