Mrengo wa kulia washinda uchaguzi Italia
26 Septemba 2022Hii ni baada ya kuongoza muungano wa kihafidhina kupata ushindi katika uchaguzi uliofanyika Jumapili.
Matokeo ya mwisho ya kura hiyo yanaonyesha muungano wa mrengo wa kulia na kati ukiwa umejikingia asilimia 44 ya kura za bunge ambapo chama cha Ndugu wa Italia kikipata asilimia 26 na vyama vyengine tanzu kama kile cha kinachopinga wahamiaji cha Matteo Salvini kikipata asilimia 9 na kile cha Forza Italia chake Silvio Berlusconi chenye msimamo wa kadri, kikipata asilimia 8.
Hatua hii inaipatia Italia fursa nadra ya uthabiti wa kisiasa baada ya miaka kadhaa ya vuta ni kuvute na miungano hafifu.
Raia wa Italia wamechagua serikali wanayoitaka
Idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa asilimia 64, hiyo ikiwa ni idadi ndogozaidi katika historia ya watu waliojitokeza kushiriki zoezi hilo. Waandaaji wa kura za maoni wanasema baadhi ya wapiga kura hawakujitokeza kama ishara ya kuonyesha kupinga kwao hatua ya kuundwa kwa serikali tatu zilizopita kabla uchaguzi uliopita ambapo wanasema jambo hilo lilifanyika kinyume cha sheria.
Meloni mwenyewe katika hotuba yake ya ushindi mapema leo amesema raia wa Italia hatimaye wameamua ni nani wanayemtaka aiongoze nchi yao.
"Tutaunda serikali thabiti, jumuishi na ambayo uwezo wake unatoka kwa raia. Serikali hii itasalia madarakani kwa kipindi cha miaka mitano, mrengo wa kushoto upende usipende," alisema Meloni.
Meloni na wenzake lakini wanakabiliwa na msururu wa changamoto ikiwemo ongezeko la bei ya nishati, vita vya Ukraine na kudorora kwa uchumi wa Italia ambao ni wa tatu mkubwa katika kanda ya Ulaya.
Mwasisi wa Umoja wa Ulaya sasa anaongozwa na chama cha mrengo wa kulia
Serikali yake ya muungano ambayo ni ya 68 nchini Italia tangu mwaka 1946 ingawa haitoidhinishwa hadi mwishoni mwa mwezi Oktoba na kabla wakati huo, Waziri Mkuu Mario Draghi ataendelea kukaimu nafasi hiyo.
Hatua ya mrengo wa kulia kuchukua uongozi wa Italia imegeuza hali halisi kuhusiana na siasa za kikanda za Ulaya, ambapo chama kinachoupinga Umoja wa Ulaya sasa ndicho kinachoongoza nchi mojawapo iliyouasisi umoja huo.
Viongozi wa mrengo wa kulia kote barani Ulaya wameusifu ushindi wa Meloni na kuibuka kwa chama chake wakisema huo ni ujumbe unaotumwa kwa Umoja wa Ulaya.
Chanzo: AFP/Reuters