Mpango wa EU wa kuokoa uchumi wa Tunisia
15 Juni 2023Mustakabali wa uhusiano kati ya Ulaya na Tunisia huenda ukaamuliwa ndani ya wiki mbilizi zijazo. Ndani ya muda huo, kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Juni, Rais wa Tunisia, Kais Saied atalazimika kuamua iwapo ataukubali "Mpango wa Ushirikiano" uliopendekezwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.
Mapema wiki hii, von der Leyen alipendekeza mpango wa msaada wa kiuchumi wa euro milioni 900 kwa Tunisia, pamoja na euro nyingine milioni 150 kwa ajili ya usaidizi wa haraka wa bajeti na euro milioni 105 ili kusimamia mipaka na shughuli za kupambana na biashara za magendo.
Kipengele cha mwisho cha msaada huo, haswa kinazungumzia jukumu linalowezekana la Tunisia kusimamia na kudhibiti uhamiaji kutoka Afrika Kaskazini hadi Ulaya. Hamza Maddeb, mtafiti mwenza wa kituo cha Carnegiw, Mashariki ya Kati, ameiambia DW kwamba msaada huo uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya utaleta utulivu wa uchumi wa Tunisia.
"Kile ambacho Umoja wa Ulaya inatoa kwa hakika ni ushirikiano kamili wa Tunisia katika suala la uhamiaji pamoja na Tunisia kuwapokea tena wahamiaji waliokataliwa wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara."
Pendekezo hilo limetolewa siku chache baada ya rasimu ya mageuzi ya uhamiaji Ulaya ambayo inataka kuiruhusu Italia kuwapeleka kwenye nchi kama Tunisia, watu wanaoomba hifadhi na wahamiaji.
Huku pwani ya Italia ikiwa umbali wa kilomita 150, Tunisia imekuwa kitovu kikuu cha wahamiaji wanaoelekea Ulaya. Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Italia, takribani wahamiaji 53,800 tayari wamefika katika fukwe zake wakitokea Tunisia kwa mwaka huu. Idadi hiyo ni mara mbili zaidi ya mwaka wote wa 2022. Wengi wa wahamiaji hao walifika kwa msaada wa watu wanaofanya biashara haramu ya kuuza binaadamu, ambao wanazingatia zaidi faida kuliko usalama.
Kulingana na Shirika ya Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, watu wapatao 1,000 walikufa au walitoweka katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2023, ikilinganishwa na 690 katika kipindi sawa na hicho mwaka 2022.
Akiwa mjini Tunis, hivi karibuni, Von der Leyen alisema Umoja wa Ulaya na Tunisia wote wana nia kubwa ya kuivunja mitandao ya biashara hiyo haramu ya kuuza binadamu.
Bonyeza story hii: Tunisia yaonya kuhusu uchumi wake kuporomoka
Mohamed Hamed, mkimbizi wa Sudan anayesubiri kupewa visa yake ya Umoja wa Ulaya, ana wasiwasi iwapo mpango huo uliopendekezwa utaimarisha hali hiyo. Ameiambia DW inasikitisha kwamba makubaliano yoyote kati ya Tunisia na Umoja wa Ulaya yatakavyokuwa, watakaoshindwa zaidi bado watakuwa wahamiaji na wakimbizi.
Jukwaa la Kiuchumi na Haki za Kijamii la Tunisia, FTDES limesema maelezo ya mapendekezo hayo sio mapya. Msemaji wa jukwaa hilo, Romdhane Ben Omar ameiambia DW kwamba ujumbe wa Ulaya umewasilisha pendekezo ambalo liliwasilishwa hapo awali mnamo mwaka 2014, na wakati huo Tunisia ililikataa, lakini sasa limerejeshwa tena.
Hata hivyo, nia ya Rais Saied kujihusisha sasa inaweza kuwa kubwa kuliko mwaka 2014. Kwa sasa uchumi wa Tunisia unadorora kwa kasi. Kulikubali pendekezo hilo kunaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi ya Tunisia, lakini ili kupata makubaliano ya Umoja wa Ulaya, na pesa zitakazoingia, Saied anapaswa kwanza kuruka kikwazo kingine.
Pendekezo la Umoja wa Ulaya linafungamana na makubaliano ya mkopo wa euro bilioni 1.7 kati ya Tunisia na Shirika la Fedha Duniani, IMF. Mpango huo umekwama kwa miezi kadhaa baada ya kukataliwa na chama kikuu cha wafanyakazi cha Tunisia chenye ushawishi mkubwa pamoja na Rais Saied mwenyewe, ambaye alitaka marekebisho kwenye vipengele ambavyo aliona havitowanufaisha wananchi. Soma-Rais wa Tunisia akataa masharti ya IMF kuhusu mkopo
Wakati huo huo, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Human Rights Watch linauona mpango wa uhamiaji unaopendekezwa kama usiokubalika. Lauren Seibert mtafiti katika kitengo cha haki za wakimbizi na wahamiaji kwenye shirika hilo, anasema kila mtu ana haki ya kuondoka katika nchi yoyote, ikiwemo nchi yao, na kila mtu ana haki ya kutafuta hifadhi, hivyo kujaribu kuwazuia watu kuondoka, kunakiuka haki hiyo.
Seibert anasema tayari Umoja wa Ulaya umekuwa ukitumia mamilioni ya euro kusaidia kile inachokiita 'usimamizi wa uhamiaji', ambao kimsingi ni kudhibiti uhamiaji na mipaka nchini Tunisia.
Sasa anahofia fedha kutoka kwenye mpango wa uhamiaji uliopendekezwa utaimarisha vikosi vya usalama vya Tunisia, ikiwemo polisi na walinzi wa kitaifa wa baharini, ambao anasema wote wamekuwa wakifanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi.