Mpango wa Biden wa kusitisha mapigano Gaza bado kizungumkuti
3 Juni 2024Hilo limeshuhudiwa wakati mapigano makali yanaendelea kwa siku ya tatu tangu Biden alipotoa hotuba yake katika Ikulu ya Marekani.
Biden, aliwasilisha kile alichokiita mpango wa awamu tatu wa Israel utakaohitimisha mzozo mbaya kabisa, kuwachiliwa mateka na kuongoza ujenzi mpya wa Gaza bila ya udhibiti wa Hamas.
Hata hivyo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisisitiza siku ya Jumamosi kwamba wataendelea na vita hadi malengo yao yatakapofikiwa, ikiwa ni pamoja na kulisambaratisha kundi la Hamas.
Msemaji wa masuala ya usalama wa White House John Kirby amesema jana kwamba wana matumaini makubwa kwamba ikiwa Hamas watakubaliana na pendekezo hilo, Israel pia itakubali.
Lakini mashambulizi yanayoendelea sasa hayatoi ishara kwamba vita hivyo vinapungua, wakati jeshi la Israel mapema leo likisema limeshambulia zaidi ya maeneo 50 kwenye Ukanda wa Gaza, kwa muda wa siku moja.