Moldova yaridhia kwa wingi mdogo kujiunga na EU
21 Oktoba 2024Rais wa Moldova, Maia Sandu, anayeunga mkono Umoja wa Ulaya, ametangaza leo kwamba kambi yake imeshinda katika mapambano yasiyo ya haki, na kusisitiza kuwa kulikuwa na jaribio la kuharibu demokrasia na kuathiri matokeo ya uchaguzi. Sandu anamtuhumu kigogo anaediwa kufadhiliwa na Urusi kula njama ya kuvuruga zoezi hilo.
Kura zilizohesabiwa zinaonyesha asilimia 50.39 ya wapiga kura wamekubali kujiunga na Umoja wa Ulaya, wakati asilimia 49.61 wamepinga. Kura ya "Hapana" ilikuwa inaonekana kuwa mbele hadi kura elfu chache za mwisho zilipohesabiwa kutoka kwa raia wengi wanaoishi nje ya nchi.
Soma: Moldova yagawanyika katika kura ya maoni ya kujiunga na EU
Kushindwa kwa kambi ya ndiyo kungekuwa janga la kisiasa kwa serikali inayoelemea Magharibi, ambayo iliunga mkono kwa nguvu kampeni ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hii ndiyo hali iliyowakabili viongozi wa serikali, ikiwemo Rais Maia Sandu, ambaye alidai kuwa kuna makundi ya wahalifu yanayojaribu kuharibu mchakato wa uchaguzi.
Katika mkutano wa waandishi wa habari, Rais Sandu amesisitiza kuwa kulikuwa na udanganyifu wa kura na uingiliaji wa kigeni, akisema mfumo wa sheria haukufanya vya kutosha kuzuia vitendo vya ufisadi. Amesema, wanahitaji kuchora mstari, kurekebisha yaliyokwenda vibaya, na kujifunza somo.
"Kilichotokea jana, lakini pia katika miaka miwili iliyopita, ni shambulio dhidi ya demokrasia na uhuru wa watu wetu, shambulio dhidi ya matarajio ya watu wetu kuwa sehemu ya familia ya Ulaya, ya amani. Maadui wa watu wetu wanataka Moldova iliyogawanyika, yenye hofu. Wanataka watu wa Moldova watilie shaka nguvu na umoja wao. Majambazi wanaotaka kurejea madarakani kwa gharama yoyote walitaka kutumia demokrasia kama udhaifu."
Scholz kuizuru Moldova na kujadili athari za vita vya Urusi nchini Ukraine
Serikali ya Moldova inadai kwamba Moscow imeongeza juhudi zake katika kampeni ya "vita mseto" ili kuyumbisha utulivu wa nchi na kuzuia juhudi zake za kujiunga na Umoja wa Ulaya. Tuhuma hizi zinajumuisha ufadhili wa makundi ya upinzani yanayoipigia debe Urusi, kueneza taarifa za upotoshaji, kuingilia kati uchaguzi wa ndani, na kuunga mkono mpango mkubwa wa ununuzi wa kura.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani atarajiwa kuwasili Moldova
Mjini Brussels, Tume ya Ulaya imesema inaunga mkono Moldova katika juhudi zake za kujiunga na Umoja wa Ulaya, huku ikisisitiza kuwa uchaguzi huo ulifanyika chini ya uingiliaji wa Urusi. Msemaji wa Tume hiyo, Peter Stano, amesema kulikuwa na vitendo vya ununuzi wa kura na uhamasishaji wa wapiga kura kwa njia zisizo halali.
Katika uchaguzi wa rais, Rais Sandu alijipatia asilimia 42 ya kura, lakini hakuweza kupata wingi wa kutosha, na hivyo atachuana na mpinzani wake, Alexandr Stoianoglo, katika duru ya pili ya uchaguzi tarehe 3 Novemba.
Kwa jumla, zaidi ya wapigakura milioni 1.5 walijitokeza kupiga kura, ikiwa ni asilimia 51 ya wapiga kura waliojiandikisha. Hata hivyo, wataalam wanatabiri kuwa upinzani wa ndani dhidi ya kujiunga na Umoja wa Ulaya unaweza kuwa na matokeo mabaya katika mustakabali wa kisiasa wa Moldova.
Moldova, nchi iliyo na wakazi wapatao milioni 2.5, iliomba kujiunga na Umoja wa Ulaya mwaka 2022 kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine. Hadi sasa, imepata hadhi ya kuwa mgombea na mazungumzo ya uanachama yameanzishwa.