Mkutano wa UN kuhusu Afghanistan wafunguliwa Doha
1 Julai 2024Mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Mataifa unaoiangazia Afghanistan umeanza jana jioni huko Doha na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka takriban nchi 30 na mashirika ya kimataifa.
Mkutano huo wa faragha unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na serikali ya Taliban na unajumuisha wajumbe wa Taliban kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwao madarakani.
Ujumbe wa Taliban, ukiongozwa na msemaji mkuu Zabihullah Mujahid, ulifanya majadiliano ya awali na wawakilishi kutoka nchi kama Urusi, India, na Saudi Arabia kabla ya mkutano mkuu. Maafisa wa Taliban walikataa kushiriki mkutano kama huo mnamo mwezi Februari.Taliban yakosolewa kwa kuwatenga wanawake katika mazungumzo na UN
Wakati Umoja wa Mataifa umekuwa ukishinikiza ajenda pana zaidi ikiwa ni pamoja na haki za binadamu, haki za wanawake, na ushirikishwaji wa kisiasa, kundi la Taliban bado linahofia ushawishi kutoka nje.