1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Mkutano wa Kim na Putin unatoa muelekeo wa malengo ya Kim

13 Septemba 2023

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Urusi Vladmir Putin walikutana katika kituo cha kurushia vyombo vya anga za juu katika mkutano wao wa kwanza wa kilele ndani ya muda wa miaka minne.

https://p.dw.com/p/4WIHK
Russland | Treffen Kim Jong Un und Wladimir Putin
Rais wa Korea Kaskazini Kim John Un na rais wa Urusi Vladimir Putin wakizungumza wakati wa mkutano wao Vostochny cosmodrome nchini UrusiPicha: Vladimir Smirnov, Sputnik, Kremlin Pool Photo via AP/picture alliance

Mazungumzo kati ya viongozi hao wa mataifa mawili yaliotengwa na yenye nguvu za nyuklia yalidumu kwa zaidi ya masaa manne na yalijikita juu ya kutanua ushirikiano wa kijeshi kati ya mataifa hayo mawili katika kuzidisha makabiliano na mataifa ya magharibi.

Uamuzi wa kukutana Vostochny Cosmodrome, ambacho ni kituo kikuu cha kurushia satelaiti, unaweza kuwasiliana kile ambacho Kim anakiona kama hatua muhimu inayofuata katika juhudi zake za kujenga ghala la silaha za nyuklia ambalo linaweza kuitishia Marekani na washirika wake barani Asia.

Kim Jong Un awasili Urusi kwa mkutano na rais Putin

Wataalamu wanasema hatua ya Kim kujigamba kwa shehena ya silaha za Korea Kaskazini ambazo yumkini Putin akazitaka kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini huenda alitafuta msaada wa kiuchumi unaohitajika sana pamoja na teknolojia ya kisasa ya silaha ili kuendeleza mpango wake wa kijeshi wa nyuklia.

Kim angeweza kushinikiza uhamishaji wa teknolojia ya Urusi kwenye satelaiti za uchunguzi wa kijeshi, nyenzo muhimu kwenye orodha yake ya matakwa ya silaha ambayo amepata shida kuipata. Kundi la maafisa wa kijeshi ambao Kim alichagua kwa safari hiyo pia wanadokeza kwamba Korea Kaskazini inaweza kutafuta teknolojia zinazohusiana na makombora na manowari zenye uwezo wa nyuklia.

Kim Jong Un: Ziara ya Urusi inaonyesha umuhimu wa kimkakati wa uhusiano wetu

Lakini bado haijulikani ikiwa Urusi itakuwa tayari kutoa teknolojia nyeti kama hizo kwa kile ambacho kinaweza kuishia kuwa kiasi kidogo cha silaha za Korea Kaskazini zinazotolewa polepole kupitia kiunga kidogo cha nchi kavu kati ya nchi hizo.

Ziara ya Kim nchini Urusi ilikuja baada ya Korea Kaskazini kushindwa mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni kupeleka satelaiti yake ya kwanza ya kijasusi wa kijeshi kwenye obiti. Nchi hiyo imeapa kufanya jaribio la tatu la kurusha satelaiti hiyo ya kijasusi mwezi Oktoba.

Huenda Kim anadhamiria kuimarisha uwezo wa Satelaiti zake

Moja ya Satelaiti za Urusi wakati ilipokuwa inarushwa angani
Moja ya Satelaiti za Urusi wakati ilipokuwa inarushwa anganiPicha: Roscosmos Press Office/TASS/dpa/picture alliance

Lakini kuna maswali juu ya iwapo satelaiti yake mpya iliyotengenezwa itakuwa ya kisasa vya kutosha kwedanana na malengo yake yaliyotajwa ya ufuatiliaji wa kina wa harakati za kijeshi za Marekani na Korea Kusini katika muda halisi na kuchakata na kusambaza picha zenye ubora wa juu.

Baada ya kuopa na kuchunguza mabaki kufuatia kushindwa kwa urushaji wa kwanza wa Korea Kaskazini mwezi Mei, jeshi la Korea Kusini lilihitimisha kuwa kifaa hicho hakikuwa na uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi wa kijeshi kutoka angani kama Kaskazini ilivyodai.

Kim Jong Un anafanya ziara kwa mshirika wake Urusi

Ujumbe wa Korea Kaskazini nchini Urusi ulimjumuisha Pak Thae Song, mwenyekiti wa kamati ya sayansi na teknolojia ya anga za juu inayoshughulikia mradi wa satelaiti za kijasusi, hatua inayoashiria uwezekano kuwa Kim alitaka kupata msaada wa Urusi katika kutengeneza mifumo hiyo. Satelaiti za kijasusi ni miongoni mwa mifumo mikuu ya silaha ambayo Kim aliapa kuitengeneza hadharani wakati wa mkutano mkuu wa kisiasa mnamo 2021.

Baada ya kushindwa mara kadhaa, Korea Kaskazini ilipeleka satelaiti yake ya kwanza angani mwaka 2012, na ya pili mwaka 2016, lakini wataalamu wanasema hakujawa na ushahidi kwamba satelaiti hizo mbili zimewahi kurejesha picha kwa Korea Kaskazini. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea Korea Kaskazini vikwazo kuhusiana na uzinduzi wa nyuma wa satelaiti, likiziona kama kificho cha makombora yake ya masafa marefu.

Alipoulizwa iwapo Urusi ingeisaidia Korea Kaskazini kujenga satelaiti, Putin alinukuliwa na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi akisema, "ndiyo sababu tumekuja hapa." Baadhi ya wachambuzi wanasema pia Kim huenda akaitaka Urusi kusaidia katika utengenezaji wa makombora ya masafa marefu na nyambizi za nyuklia. Alisafiri pia na kamanda wake wa juu wa jeshi la majini, Admiral Kim Myong Sik.