1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Kim Jong Un anafanya ziara kwa mshirika wake Urusi

Hawa Bihoga
12 Septemba 2023

Korea Kaskazini imethibitisha leo Jumanne kuwa kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un aliondoka mjini Pyongyang Jumapili alasiri na kuelekea nchini Urusi kwa kutumia treni ya kivita.

https://p.dw.com/p/4WDkB
Nordkoreas Führer Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akiwasili Urusi leo asubuhiPicha: Korean Central News Agency/Korea News Service/AP/picture alliance

Taarifa hiyo imetolewa na shirika la habari linalodhibitiwa na serikali la KCNA waki nukuu wizara ya ulinzi ya Korea kaskazini.

Jana, Ikulu ya Kremlin ilithibitisha mkutano uliopangwa kati ya Kim na Rais Vladimir Putin katika mji wa Vladivostok nchini Urusi, taarifa iliyotolewa hapo awali na gazeti la Marekani la New York Times wiki iliyopita.

Kim Jong Un ambaye hutoka mara chache nchini mwake anatarajiwa kukutana na Putin kujadiliana makubaliano muhimu ya silaha ambazo Moscow inazihitaji kuendeleza vita vyake nchini Ukraine.

Soma pia:Ikulu ya Kremlin imesema Kim Jong Un atazuru Moscow katika siku za hivi karibuni kufuatia mwaliko wa Vladimir Putin

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema mkutano wa Putin na Kim utafanyika Mashariki mwa Urusi, ingawa mwanzoni haikufahamika mahali hasa mkutano huo ungelifanyika.

Peskov alisema kutakuwa na mikutano kati ya viongozi hao wawili na mazungumzo ya moja kwa moja kabla ya chakula cha jioni rasmi.

Mazungumzo yatalenga vita vya Ukraine?

Gazeti la The Times liliripoti kwamba Kim anapanga kujadiliana kuhusu ugavi wa silaha na Putin.

Moscow ina wasiwasi wa ugavi wa silaha kwa ajili ya vita vyake dhidi ya Ukraine.

Bildkombo | Geplantes Treffen zwischen Putin und Kim Jong Un
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: Uncredited/Pool Sputnik Kremlin/KCNA via KNS/AP/dpa/picture alliance

Gazeti hilo lilisema Putin anatarajia makombora ya Korea Kaskazini na silaha za kupambana ikiwemo vifaru.

Upande wa Kim kwake ana matumaini ya maendeleo ya teknolojia ya satelaiti na nyambizi zinazotumia nyuklia, pamoja na msaada wa chakula.

Kufuatia uthibitisho wa mkutano wa viongozi hao wawili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema, Washington inayo haki ya kuweka vikwazo zaidi kwa Urusi na Korea Kaskazini kutokana na mazungumzo yaliyopangwa kuhusu uwasilishaji wa silaha, kwa urusi.

Soma pia:Rais wa Urusi Vladmir Putin atoa wito wa kuimarisha ushirikiano katika nyanja zote na Korea ya Kaskazini

Washington ilisema siku ya Jumatatu kwamba uhamisho wowote wa silaha kutoka Korea Kaskazini hadi Urusi ni ukiukaji wa maazimio mengi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Ukweli ni kwamba Urusi inalazimika kuiomba msaada wa kijeshi Korea kaskazini,"

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Marekani Matthew Miller alisema siku ya Jumatatu.

"Hii ni kutokana na ufanisi wa vikwazo vyetu,udhibiti wa usafirishaji silaha."Alisisitiza.

Urusi ni mshirika wa siku nyingi wa Korea Kaskazinina Kim amekuwa Urusi mara moja tu, alipotembelea Vladivostok mnamo Aprili 2019 - akitumia  treni yake ya kivita.

Korea Kaskazini yafyatua tena makombora

Wakati huo, mazungumzo yao yalilenga mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini na uimarishaji wa ushirikiano wa kiuchumi.

Walakini, hakukuwa na matokeo madhubuti.