MKUTANO WA G 20 UNAANZA LEO MJINI CANNES
3 Novemba 2011Mkutano wa kilele wa nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi unaanza leo katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Kwenye mkutano huo wa siku mbili viongozi wa nchi hizo wataijadili mikakati ya kuleta ustawi wa uchumi na kutenga nafasi za ajira.
Rais Barack Obama ameshawasili katika mji wa Cannes ili kuungana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais Sarkozy wa Ufaransa na viongozi wengine kwa ajili ya mkutano huo. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika wakati ambapo mzozo mkubwa umezuka juu ya Ugiriki.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo George Papandreou ametangaza kufanyika kura ya maoni ili kuamua juu ya msaada unaokusudiwa kutolewa na nchi nyingine za Ulaya kwa ajili ya kuikoa nchi yake.
Ujerumani inayowakilishwa na Kansela Merkel kwenye mkutano huo inataka nchi zote zifuate sera imara za bajeti sambamba na kudhibitiwa kwa masoko ya fedha. Ujerumani pia inataka kuazishwa kodi katika shughuli za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Rais Obama anatumai kwamba mkutano wa mjini Cannes utatoa ishara zitakazochangia katika kuutia msukumo uchumi wa nchi yake. Obama amekutana na mwenyeji wa mkutano Rais Sarkozy wa Ufaransa kabla ya kuanza rasmi kwa mkutano wa nchi 20. Rais Obama na Rais Sarkozy walitembea kwa pamoja na kuwasilimu na kupeana mikono na watu.
Rais Sarkozy anatumai kuitumia fursa ya mkutano ili kuipitisha ajenda juu ya kuanzisha taratibu mpya za udhibiti wa mabenki. Hata hivyo mgogoro wa madeni unaozikabli nchi kadhaa za Ulaya ndilo litakalokuwa suala la kipaumbele kwenye mkutano wa mjini Cannes.
Mazungumzo ya viongozi kutoka nchi hizo 20 muhimu duniani yanatarijiwa kuanza muda mfupi kuanzia sasa kwa chakula cha mchana ambapo hali ya uchumi wa dunia kwa jumla itajadiliwa. Hapo baadae viongozi hao watayajadili masuala ya biashara, fedha na utawala bora duniani.
Mwandishi/Paulet Rüdieger/ARD/ZDZ/
Tafsiri/Mtullya Abdu/
Mhariri/ Josephat Charo