Mkanyagano nchini Yemen wasababisha vifo vya watu 85
20 Aprili 2023Mamia ya watu kwenye taifa hilo linalokabiliwa na umasikini walikuwa wamekusanyika katika shule moja iliyoko mji mkuu, Sanaa kwa ajili ya kugawiwa fedha kiasi cha dola 8 za Marekani za kujiendesha kimaisha. Picha za video zilizorushwa na kituo cha televisheni cha Al Masirah zimeonyesha miili iliyorundikana na watu wakiwa wanakanyagana na kusukumana wakitafuta upenyo wa kupita.
Watu waliokuwa na silaha na waliovalia nguo za kijeshi na waliokuwa wakigawa msaada huo, baadae walionekana wakilipigia kelele kundi hilo la watu wakiwataka kurudi nyuma, huku wakiwasukuma kujaribu kuepusha mkanyagano zaidi.
Kwenye mkanyagano huo, karibu watu 85, ikiwa ni pamoja na watoto wamefariki na 322 walijeruhiwa katika tukio hilo lililotokea kwenye wilaya ya Bab al-Yemen, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa kundi la wanamgambo wa Houthi ambaye hakutaka kutambulishwa na kuongeza kuwa 50 miongoni mwao walikuwa na hali mbaya. Idadi kama hiyo imethibitishwa pia na afisa mwingine wa afya.
Mawaziri wa serikali ya Kihouthi wametembelea eneo la tukio hilo na kutangaza kamba uchunguzi unaendelea ili kujua kilichosababisha kisa hicho. Waziri mkuu wa vuguvugu la Houthi nchini Yemen Abdulaziz Bin Habtour, amewaambia waandishi wa habari kwamba mamlaka husika zimeendelea na kuchunguza kisa hicho na kwa sasa wanachukua hatua stahiki ili kuwashughulikia kwanza majeruhi wa wahanga wa tukio hilo.
"Waziri wa mambo ya ndani, ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali na mkuu wa Baraza la Juu la Mahakama pamoja na maafisa wengine muhimu wameendelea na majukumu yao ya kisheria kuchunguza tukio hili baya na kupata suluhu madhubuti ili kuhakikisha halijitokezi tena," alisema Habtour.
Kulingana na mkuu wa Tume ya Juu ya Kimapinduzi ya Houthi Moammed Ali al-Huthi, tukio hilo lilisababishwa na mrundikano mkubwa wa watu. Amesema watu hao walikuwa wamerundikana kwenye mtaa mwembamba unaoelekea kwenye shule hiyo na mara baada ya lango kuu kufunguliwa, kundi hilo lilivamia kwa nguvu kupitia ngazi nyembamba zinazoelekea eneo kulikokuwa kunatolewa fedha hizo.
Soma Zaidi: UNICEF: Watoto milioni 11 wanategemea misaada ya kiutu Yemen
Mmoja ya mashuhuda hata hivyo amesema, milio ya risasi iliyolenga kuwatawanya watu, pia iliwashtua wengi.
Baada ya tukio hilo, familia nyingi zilikusanyika kwenye hospitali mbalimbali, lakini wengi hawakuruhusiwa kuingia, kwa kuwa maafisa wa ngazi za juu pia walikuwa wakiingia kuwaona majeruhi na waliofariki.
Muda mfupi baada wanajeshi wa vikosi vya usalama waliojihami kwa silaha waliepelekwa mara moja kwenye shule kulikotokea mkanyagano, na walionekana kuwazuia jamaa wa wahanga kuingia shuleni hapo ili kuwatambua ndugu zao.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miaka minane nchini Yemen vimesababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mzozo mbaya kabisa wa kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni. Mzozo huo ulioanza mwaka 2014, baada ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kuukamata mji mkuu Sanaa, uliongezeka baada ya muungano wa kijeshi ulioongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati. zaidi ya watu milioni 21.0 nchini humo wanahitaji misaada ya kiutu kwa mwaka huu kutokana na umasikini mkubwa uliochangiwa na vita hivyo.