1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN Afghanistan aomba kubaki kwenye nafasi yake

17 Septemba 2021

Balozi wa Umoja wa Mataifa anayeiwakilisha serikali ya Afghanistan iliyoondolewa madarakani ameomba kubakia katika nafasi yake, kwa hofu ya kuzuka mgongano iwapo uongozi wa Taliban utajaribu kumteua mjumbe wake.

https://p.dw.com/p/40T0r
G-20 Gipfel in Matera
Picha: Angelo Carconi/ANSA/REUTERS

Balozi Ghulam Isaczai amesaini barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres huku akiambatanisha orodha ya ujumbe wa Afghanistan utakaohudhuria mkutano wa Baraza Kuu wa Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema balozi huyo alituma ombi lake la idhini Jumatano, siku moja baada ya kikao kipya cha Baraza Kuu kuanza.

Haijafahamika wazi iwapo kundi la Taliban lililochukua madaraka mwezi uliopita baada ya majeshi ya Marekani kuondoka, litampeleka mjumbe wake katika mkutano huo. Wiki ijayo viongozi kadhaa wa dunia wataelekea New York, Marekani kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu wa Umoja wa Mataifa na Isczai anatarajiwa kuhutubia siku ya mwisho ya mkutano huo Septemba 27.

Italia na mkutano wa G20 kuhusu Aghanistan

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Italia, Luigi Di Maio amesema nchi hiyo bado inapanga kuandaa mkutano maalum wa kundi la nchi zilizostawi na zinazoinukia kiuchumi za G20 utakaoizungumzia hali nchini Afghanistan. Di Maio amesema mkutano wa G20 utafanyika baada ya mkutano wa Baraza Kuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York.

Serikali ulimwenguni zinaangalia jinsi ya kushirikiana na Taliban baada ya kuchukua madaraka, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa mzozo wa kibinaadamu. Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi mwenyekiti wa G20 kwa mwaka huu, amekuwa akijaribu kuandaa mkutano maalum wa kilele, tangu Taliban ilipochukua madaraka.

Russland | Moskau | PK Angela Merkel und Wladimir Putin
Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/imago images

Huku hayo yakijiri, Urusi, China, Pakistan na mataifa mengine ya kanda ya Asia ya Kati na Ulaya Mashariki zimeitaka Marekani kushirikiana na Taliban na kuisaidia Afghanistan, ingawa pia wametoa wito kwa wapiganaji wa zamani kuufanya utawala nchini humo kuwa wa jumuishi. Mustakabali wa Afghanistan ulitawala kwenye mkutano wa kilele wa Shirika la Ushirikiano wa Shanghai.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema sehemu kubwa ya gharama zinazohusiana na kuijenga upya Afghanistan zinatakiwa kubebwa na Marekani. Putin ameitaka Marekani kuziachia mali za Benki Kuu ya Afghanistan.

''Katika suala hili, nadhani tunapaswa kushirikiana na Marekani na nchi nyingine za Magharibi kuziachia polepole akiba za kifedha za Afghanistan na kurejesha miradi kupitia Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani,'' alifafanua Putin.

Nchi zinapaswa kuchukua majukumu yao

Naye Rais wa China, Xi Jinping amesema nchi kadhaa zinapaswa kuchukua majukumu yao kwa maendeleo ya baadae ya Afghanistan, kwa sababu wamekuwa wachochezi wa hali hiyo. Xi alizungumza hata hivyo bila ya kuitaja Marekani.

Kwa upande mwingine wizara ya elimu ya Taliban imesema wanafunzi wote wa kiume wa darasa la sita hadi 12 na walimu wa kiume wanapaswa kurejea shuleni kuanzia kesho. Taarifa hiyo ambayo imechapishwa leo kwenye mtandao wa Facebook, haikuwajumuisha wanafunzi wa kike wenye umri kama huo na kutokana na kukosekana kwa mwongozo, kunaendeleza wasiwasi uliopo kwamba huenda Taliban wakaweka masharti kwa wasichana na wanawake.

Mbali na hayo, Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier leo amemtunukia Tuzo ya Juu ya Heshima ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Brigedia Jenerali Jens Arlt, aliyeongoza operesheni ya kuwaondoa watu nchini Afghanistan.

(DPA, AFP, AP, Reuters)