Wanawake wakatwa katwa na kutupwa dampo Nairobi
12 Julai 2024Polisiwalifyatua kwa muda mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kutawanya kundi la watu wenye hasira waliokusanyika kwenye kituo cha polisi karibu na eneo la ugunduzi huo mbaya eneo la Mukuru, kusini mwa mji mkuu, alisema mwandishi wa shirika la habari la AFP.
"Tahadhari ilitolewa kufuatia kugunduliwa kwa miili sita iliyoharibika vibaya, yote ya wanawake, ikiwa katika hatua mbalimbali za kuoza," Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ilisema katika taarifa yake.
Soma pia: Kenya yatimiza mwaka mmoja tangu mauaji ya Shakahola
"Miili hiyo ilikuwa imefungwa kwa mifuko ya nailoni na kukazwa kwa kamba za nailoni pia." Mashuhuda walikuwa wameripoti awali kwamba miili tisa ya wanaume na wanawake ilikuwa imepatikana.
Wapelelezi wa mauaji na maafisa wa uchunguzi walikuwa katika eneo la tukio, ambalo ni machimbo yaliyotelekezwa na yaliyojaa maji na kutumika kama eneo la kutupa taka.
Raia wataka majibu ya haraka
"Tunahitaji majibu kutoka kwa polisi kwa sababu hili ni jambo linalohitaji kuchunguzwa haraka sana," alisema Lucy Njambi, amkaazi wa Mukuru.
"Inashangaza nilichokiona. Miili ilitumbukizwa kwenye magunia na kutupwa kwenye jalala."
Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alithibitisha ugunduzi huo. "Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini utambulisho na namna watu hawa walivyouawa," aliwaambia waandishi wa habari.
Soma pia: Polisi wa Kenya washutumiwa kuwaua waandamanaji 12
Ofisi ya DCI ilisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa waathiriwa wote waliuawa kwa njia sawa, bila kufafanua.
Miili hiyo imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha jiji ili kusubiri uchunguzi wa sababu za vifo vyao, iliongeza.