1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migawanyiko ndani IMF, Benki ya Dunia kuhusu vita vya Gaza

16 Oktoba 2023

Majadiliano ya viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa juu ya mashambulizi ya Hamas nchini Israel na majibu ya Israel dhidi ya mashambulizi hayo yaliyoanza wiki iliyopita yanaonesha migawanyiko mikubwa baina yao.

https://p.dw.com/p/4Xa9x
Marokko Marrakech IMF World Bank
Sehemu ya nje ya ukumbi mmPicha: Christophe Gateau/dpa

Kundi la Hamas liliishambulia Israel tarehe 7 Oktoba wakati maafisa waandamizi wa taasisi za fedha wakiwasili Morocco kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

Mkutano huo ulianza kwa tahadhari kubwa na kutolewa kwa miito ya fedha zaidi na hatua za kufufua ukuaji wa uchumi wa dunia unaoyumba.   

Mkurugenzi mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva, hakuutaja mgogoro huo mpya katika ufunguzi wa mkutano wao wa kila mwaka, lakini baadaye wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, Georgieva akalizungumzia suala hilo na kulitaja kama janga la kibinaadamu na chanzo kisicho wazi cha kukosekana kwa utulivu wa kiuchumi.

Soma zaidi: IMF yalazimisha ufadhili kupambana na umasikini

Washiriki katika mkutano huo waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba katika majadiliano ya faragha, mgogoro wa Israel na Gaza uliibuka: kuanzia mgogoro mpya wa wakimbizi unaosababishwa na vita hivyo, athari za kibiashara na kitisho cha mapigano nchini Lebanon na katika Ukingo wa Magharibi. 

Kiwingu kwenye mafanikio ya mkutano wa IMF, WB

Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga alikiri siku ya Jumapili (Oktoba 15) kwamba mgogoro wa Israel na Hamas, pamoja na vita vya Ukraine na mapigano yanayoendelea katika sehemu tofauti za Afrika yanasababisha kiwingu kikubwa katika mafanikio ya mkutano huo na kuongeza changamoto za kiuchumi zilizopo. 

USA IWF Kristalina Georgieva
Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva, (kulia) akizungumza na waandishi wa habari.Picha: Liu Jie/Xinhua/IMAGO

Banga amesema bila amani ni vigumu kwa watu kufikia uthabiti, ukuaji, kuwaangalia watoto wao na hata kupata ajira. 

Hata hivyo, bodi ya Benki ya Dunia iliidhinisha dira mpya ya kuunda "ulimwengu usio na umasikini" ili kuenda sambamba na mkakati wake mwengine mpya wa kupambana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kuzisaidia nchi zinazoyumba kiuchumi na kuwa na mikakati mipya ya kutanua hatua zake za utoaji mikopo. 

Soma zaidi: IMF, Benki ya Dunia zafanya mikutano ya kwanza Afrika katika kipindi cha miaka 50

Josh Lipsky, aliyekuwa afisa wa IMF na ambaye sasa anaongoza Baraza linalosimamia siasa za kikanda, amesema migogoro hiyo inabakia kuwa changamoto kubwa kwa uchumi wa dunia.

"Iwapo IMF na Benki ya Dunia zitataka kuwa na uhalali na kuonekana kuwa sahihi katika kile zinachokifanya ndani ya muongo mmoja unaokuja, basi ni lazima pia watoe majibu kwa migogoro ya kikanda inayosababisha uchumi wa dunia kudorora." alisema Banga akiongeza kuwa haitowezekana kwa mataifa haya kujitenga na hali halisi inayoendelea. 

Chanzo: Reuters