Miaka 4 ya makubaliano kati ya Kenyatta na Raila
9 Machi 2022
Makubaliano hayo ya miaka 4 iliyopita yaliyofikiwa kwenye ngazi za jengo la Harambee hapa jijini Nairobi ndiyo yaliyoituliza nchi kisiasa. Kwenye mahojiano hii leo, jaji mkuu wa zamani Willy Mutunga amewashauri Wakenya kusubiria mwafaka mpya baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu.
Kwa mtazamo wake, makubaliano ya safari hii yatakuwa kati ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na naibu wa rais William Ruto. Ikiwa imesalia miezi 5 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, naibu wa rais sasa amebadili mtazamo na kukiri kuwa atayakubali matokeo.
Akiwa Marekani siku chache zilizopita, William Ruto alidai kuwa ipo njama ya kuiba kura na kwamba mwafaka huo wa 2018 ndio uliozua sintofahamu serikalini. Amesema shida ya makubaliano hayo kulikuwa na utapeli mwingi hivyo hawakukubaliana na uwamuzi huo alioutafsiri kuwa serikali ingelisambaratika "haieleweki serikali imeingia upinzani au upinzani umeingia serikalini." AlisemaRuto kwenye mahojiano wakati wa ziara yake Ughaibuni.
Soma Pia:Ruto ashutumiwa kuanza harakati za kukataa matokeo ya uchaguzi
Naibu wa rais Ruto anafanya ziara ya siku 12 ya Marekani na Uingereza. Kongamano kuu la chama cha United Democratic, UDA, cha William Ruto kilicho mwanachama mkuu wa muungano wa Kenya Kwanza limepangwa kufanyika wiki ijayo.
Itakumbukwa kuwa Mwafaka wa 2018 wa kisiasa kati ya rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Odinga ndio uliozua muungano wa Azimio la Umoja unaopigiwa upatu na kiongozi wa taifa.
Makubaliano hayo kadhalika yaliuanzisha mchakato wa BBI wa kufanya mageuzi ya katiba ila hatima yake inasubiri kauli ya mahakama ya juu baada ya kugonga mwamba.
Wandani wa Kenyatta wampigia debe Odinga rasmi
Wakati huohuo, wandani wa rais Kenyatta sasa wanampigia debe Odinga hasa katika maeneo ya Mlima Kenya anakotokea kiongozi wa taifa. Muungano wa Azimio la Umoja wa Odinga leo uko kaunti ya Wajir ikiwa ni sehemu ya ziara ya kaunti 9 ya kunadi sera.
soma Pia:Mudavadi na Ruto waungana kabla ya uchaguzi mkuu Kenya
miongoni mwa mambo walioyaahidi kwa wakaazi wa eneo hilo ni pamoja na kuleta maendeleo katika kauti hizo
Yote hayo yakiendelea, chama cha KANU kimezindua sera zake na Ilani ya chama wanaposubiria uchaguzi mkuu wa Agosti. Akizungumza kwenye bustani la Kabarnet hapa jijini Nairobi, mwenyekiti wake Gideon Moi ameahidi kuimarisha uchumi na kupambana na ufisadi moja kwa moja. Nick Salat ni katibu mkuu wa chama cha KANU.
Nacho chama cha Kiraitu Murungi kimejiunga na muungano wa Azimio la Umoja. Katika maandalizi ya uchaguzi wenyewe, Marjan Hussein Marjan amekabidhiwa rasmi wajibu wa kuiongoza tume ya IEBC baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu 2018.