1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 30 ya mauaji ya Tiananmen

4 Juni 2019

Wakati China ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 baada ya hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya waandamanaji waliounga mkono demokrasia nchini humo, rais wa Taiwan Tsai Ing-wen amesema taifa hilo bado linaficha ukweli.

https://p.dw.com/p/3JnbD
China Peking 1989 Studentenproteste Pro Demokratie
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Avery

China inadaiwa kuficha ukweli kuhusu hatua hizo zilizosababisha waandamanaji kupoteza maisha. 

Miaka 30 iliyopita vikosi vya jeshi nchini China viliwamiminia risasi waandamanaji waliokuwa wakipigania demokrasia waliokusanyika kwenye bustani ya Tiananmen mjini Beijing ili kusambaratisha maandamano hayo na kusababisha vifo ambavyo hadi sasa idadi halisi haijajulikana. Makundi ya wanaharakati yanasema mamia kwa maelfu waliuawa.

Maandamanao hayo yaliongozwa na wanafunzi. Mamlaka za China zimezuia maandamano ya umma na haijawahi kutaja idadi ya waliouawa. 

Rais Tsai Ing-wen ameishutumu serikali ya China kupitia ukurasa wa Facebook akisema sio tu kwamba ingejipanga kuomba radhi, lakini pia imeendelea kufunika ukweli na kuiambia inatakiwa kutambua kwamba Taiwan haitakubali kudhoofishwa na shinikizo kutoka kwake.

Peking 1989 Studentenproteste Pro Demokratie
Waandamanaji waliokabiliwa na hatua kali mnamo 18.05.1989 wakiunga mkono demokrasia.Picha: picture alliance/dpa/AP/S. Mikami

Jijini Beijing, serikali iliimarisha ulinzi kwenye bustani hiyo ya Tiananmen. Kumeongezwa vituo zadi vya ukaguzi na kufungwa kwa baadhi ya mitaa. Gwaride la heshima lilipita kwenye barabara zenye vizuizi hivyo huku likipeperusha bendera za China wakati wimbo wa taifa ukipigwa.

Feng Conde ambaye ni mmoja ya wanafunzi waliokuwepo kwenye maandamano hayo ya Tiananmen, alisema "Kama nisingefanya kitu kukumbuka tukio hili.... huwa nasema ni ombwe la kumbukumbu kwa sababu serikali ya China inataka kizazi kijacho kisahau kuhusu hili ama kutumia propaganda zao kupoteza ukweli wa kihistoria. kwa hiyo kwangu mimi, sio tu siku ya kumbukumbu bali huwa ndani mwangu kila siku."

Schweiz Bellinzona US-Außenminister Mike Pompeo
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo akosolewa vikali kutokana na matamshi yakePicha: picture-alliance/KEYSTONE/Ti-Press/S. Golay

Mapema, ubalozi wa China nchini Marekani umekosoa vikali matamshi ya mwanadiplomasia wa juu nchini humo Mike Pompeo kuhusiana na hatua hizo.

Pompeo kwenye taarifa yake jana Jumatatu aliwasifu wale aliowataja mashujaa wa watu wa China ambao miaka 30 iliyopita walisimama imara kupigania haki zao. Lakini pia aliitaka China kuuarifu umma kuhusu waliouawa huku akielezea kupungua kwa matumaini ya Marekani kwamba China itakuja kuwa taifa la uwazi na uvumilivu.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Jeremy Hunt imeiomba China kuwaruhusu raia wake kuandamana kwa amani na kufurahia uhuru wa kujieleza, katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo kwa kuwa hadi sasa raia nchini humo hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amezungumzia kwa mara nyingine namna Halmashauri ya Ulaya ilivyoituhumu China kwa ukandamizaji mbaya kabisa kufuatia tukio hilo la 1989 na kuelezea umuhimu wa kumbukumbu hiyo kwa ajili ya kizazi kijacho.