Meloni ataka ushirikiano ili kukabiliana na wahamiaji haramu
24 Julai 2023Akizungumza Jumapili katika Mkutano wa kilele wa Kimataifa wa Maendeleo na Uhamiaji uliofanyika mjini Roma na kuzihusisha takribani nchi 20, Meloni amesema ushirikiano mkubwa unahitajika katika ya mataifa ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaoingia Ulaya kwa msaada wa Afrika.
Mkutano huo unakusudia kuifanya Italia kuwa kiongozi katika kutatua masuala yanayoathiri mataifa yaliyoko katika Bahari ya Mediterania.
Mamia ya wahamiaji wanaingia Italia kila siku
Jambo kuu miongoni mwake ni uhamiaji, kwani Italia inawahifadhi mamia ya wahamiaji wapya wanaowasili kila siku kwenye mpaka wa kusini wa Ulaya, lakini pia nishati, huku Ulaya ikiitazama Afrika na Mashariki ya Kati kama zitakazochukua nafasi ya kudumu ya usambazaji wa Urusi.
Meloni amesema kuna uwezekano kuwa kiburi kinachoonyeshwa na mataifa ya Magharibi, kimekuwa kikwazo katika kutafuta suluhisho la suala la uhamiaji, kwa sababu yamekuwa yakitoa mapendekezo badala ya kusaidia.
Meloni amesema kuna uwezekano kuwa kiburi kinachoonyeshwa na mataifa ya Magharibi, kimekuwa kikwazo katika kutafuta suluhisho la suala la uhamiaji.
''Tunataka kukomesha uhamiaji haramu. Hadi Ulaya ifikiri kwamba inaweza kutatua suala hili kwa kujadili jinsi ya kuwadhibiti wahamiaji haramu wakishafika katika ardhi ya Ulaya, hatutoweza kamwe kupata suluhu ya kweli, kwa sababu maslahi ya mataifa yetu ya Ulaya ni tofauti,'' alifafanua Meloni.
Amependekeza njia kuu nne za ushirikiano wa siku zijazo, ikiwemo kupambana na mashirika yanayofanya biashara haramu ya kusafirisha wahamiaji, kusimamia vyema wimbi la wahamiaji, kuwasaidia wakimbizi na kuzisaidia nchi wanazotoka wahamiaji hao.
Maandalizi ya mkutano wa wafadhili
Meloni amesema mkutano huo ni mwanzo wa mchakato ambao utafuatiwa na mkutano wa wafadhili wa kufadhili miradi ya uwekezaji na kusaidia udhibiti wa mipaka. Meloni amesema Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi kutoa euro milioni 100 kwa ajili ya mfuko huo.
Akizungumza katika mkutano huo uliolenga kukomesha wimbi la wahamiaji haramu, na kupambana na biashara haramu ya kuuza binaadamu, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema wanahitaji kupambana na mitandao ya kihalifu ili kuisambaratisha kabisa.
''Tutaimarisha uratibu wetu kwenye shughuli za uokozi na utafutaji. Na tumekubaliana kwamba tutashirikiana katika usimamizi wa mipaka, kupambana na biashara za magendo, na kushughulikia kiini cha tatizo hili kwa kuheshimu sheria za kimataifa,'' alibainisha Von der Leyen.
Von der Leyen amesema pia anaona fursa kubwa za ushrikiano na Afrika Kaskazini katika uzalishaji wa nishati ya kijani, na kwamba Tunisia ina maliasili muhimu zinazohitajika za upepo na jua.
Kabla ya mkutano huo, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewataka viongozi wa Ulaya na Afrika kutafuta suluhisho la kuwasaidia maelfu ya watu ambao wamezuiliwa katika mipaka ya Afrika Kaskazini, wakiwa wanajaribu kuingia Ulaya kutafuta maisha bora, kutokana na umasikini na migogoro.
Waliohudhuria mkutano
Mkutano huo wa siku moja umehudhuriwa na viongozi wa Tunisia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Mauritania, pamoja na Von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi, pamoja na mashirika ya kimataifa.
Mkutano huo umefanyika wiki moja baada ya mmoja wa washirika muhimu, Rais wa Tunisia Kais Saied kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati, katika mkutano uliohudhuriwa na Meloni na Von der Leyen.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, zaidi ya wahamiaji 1,900 wamekufa au hawajulikani walipo na inakisiwa wamepotelea katika Bahari ya Mediterania kwa mwaka huu, na kuifanya idadi jumla kufikia 27,675 tangu mwaka 2014.