Mazunguzo ya amani ya Kenya na Ethiopia yaendelea
2 Agosti 2023Raia watatu wa Ethiopia na Mkenya mmoja walipoteza maisha yao kufuatia mzozo wa kijamii katika eneo hilo. Tukio hilo ni la kwanza kuripotiwa tangu kipindi cha ukame kukamilika mwezi Desemba mwaka uliopita.
Wizara ya usalama wa ndani imetangaza kuwa imewapeleka maafisa wa polisi katika mpaka wake na Ethiopia kwenye eneo la Dukana kufuatia hali ya taharuki inayotanda huko. Hali imekuwa ya wasiwasi tangu siku mbili zilizopita, wakati ambapo watu wanne waliuawa kwa kupigwa risasi.
Wadau wahimiza juhudi ya haraka ya amani katika eneo la Marsabit.
Wadau katika sekta mbalimbali hapa Marsabit wamekuwa wakiishinikiza serikali kuchukuwa hatua za haraka ili kuthibiti hali hiyo ambayo inahofiwa kuzua mzozo wa kikabila. Kamishna wa Marsabit, Norbert Komora amethibitisha mauaji hayo akieleza kwamba tayari maafisa wa usalama wamepelekwa kwenye eneo la mkasa ili kuthibiti hali ya usalama.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama hapa Marsabit Sora Guyo Huka, amezitaka jamii zinazoishi mpakani kudumisha amani badala ya kuvurugana na kusababisha maafa. Anasema"Kulitokea kisa ambapo kijana mwenye umri wa miaka kumi na mitano aliuawa mpakani. Wakati maiti yake ilipogundulika, vijana wakavamia upande wa Ethiopia na kutekeleza mauaji.”
Chanzo cha gadhabu za machafuko.
Tukio hilo la mauji ya watu hao limeendelea kuzusha gadhabu miongoni mwa jamii za hapa Marsabit, huku Gavana wa Marsabit Muhamud Ali akiwatolea wito wakaazi kuzika tofauti zao na kuikumbatia amani ambayo imekuwa ikishuhudiwa jimboni hapa. Gavana Ali amevitolea wito vyombo vya dola kusaidia katika kuwakamata washukiwa wa mauaji hayo.
Zaidi amenukuliwa akisema "Hata yale maneno tunayoyasikia kule Dukana, tunaomba waishi kwa amani. Na tunaomba waliotekeleza unyama huo wakamatwe na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.”
Soma zaidi:Viongozi wa kikanda wakubaliana kuiangamiza al-Shabab
Kufikia sasa, bado maafisa wa polisi wanaendelea kushika doria kwenye mpaka huo wakati serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, ikiendelea na mazungumzo kati ya jamii zinazoishi mpakani humo kama sehemu ya kuzuia kuzuka kwa vita vya kikabila.
Chanzo DW: Kenya