Mazungumzo ya Yemen yarefushwa Geneva
18 Juni 2015Mazungumzo hayo yaliyokuwa yamepangiwa kumalizika leo yameongezewa muda hadi kesho Ijumaa, baada ya hapo jana mujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen,ambaye ni mwanadiplomasia wa Mauritania,Ismail Ould Cheikh Ahmed kukutana na pande zote mbili zinazohusika kwenye mgogoro huo wa Yemen.
Cheikh Ahmed alikutana kwa nyakati tofauti na ujumbe wa waasi katika hoteli moja mjini Geneva jana jioni baada ya kumaliza mazungumzo yake na ujumbe wa serikali inayoishi uhamishoni. Kilichojadiliwa ni haja ya kusitishwa vita ingawa wahouthi wanadai suala hilo haliwezi kufanyika ikiwa upande wa pili katika mazungumzo hayo unawweka masharti yasiyokubalika.Pamoja na kizingiti mazungumzo hayo yanatajwa kupiga hatua.
''Kwa sasa tumefikia mahala pazuri naweza kusema hivyo,Tumeanza kuelekea katika njia nzuriu na tumeanzia na mambo ambayohuenda yakawa ndiyo hatua ya mwanzo ya kutufikisha mwisho wa mgogoro huu haraka.mungu akipenda,'' alisema Ali Al Imad ni mjumbe kutoka upande wa waasi wa Houthi anasema Ali Al Imad mjumbe kutoka upande wa waasi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kutoka duru za mkutano huo ni kwamba waasi wa houthi pamoja na washirika wao yaani vikosi tiifu kwa rais aliyeondolewa madarakani Ali Abdalla Saleh wanaunga mkono mapngo wa kusitisha vita ila wanapinga sharti la kuwataka kuondoka kwenye maeneo wanayoyadhibiti linalotolewa na serikali iliyoko uhamishoni inayoungwa mkono na Saudi Arabia.
Waziri wa mambo ya nje wa Yemen Riad Yassin pamoja na wajumbe wengine kutoka upande wa serikali inayoishi uhamishoni wameshikilia msimamo kwamba suala la waasi kuondoka kwenye maeneo wanayoyadhibiti halina mjadala.Ujumbe huo wa serikali jana ulikutana asubuhi na kundi la wanadiplomasia 16 kutoka nchi zenye nguvu za Umoja wa Ulaya pamoja na nchi za Ghuba zinazofuatilia mazungumzo hayo.Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen,Ould Cheikh Ahmed amesema kwa hali iliyopo katika mazungumzo hayo kuna haja ya wayemen wenyewe kukaa kwenye meza moja na kuzungumza miongoni mwao.
Hata hivyo mazungumzo ya Geneva yanaendelea wakati ndani ya Yemen kwenyewe kunaripotiwa umwagikaji wa damu aambapo inaarifiwa katika mji mkuu wa Sanaa,kiasi ya watu 31 wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi matano ya mabomu yanayodaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu dhidi ya misikiti ya washia pamoja na ofisi zao.Kundi hilo la dola la Kiislamu ambalo ni la wasunni wenye itikadi kali linasema limefanya mashambulizi hayo kulipiza kisasi dhidi ya wahuthi ambao ni washia waliotwaa udhibiti wa mji mkuu Sanaa pamoja na maeneo mengine mengi katika nchi ambayo idadi kubwa ya wakaazi wake ni Wasunni.
Yemen imetumbukia kwenye mapigano na mgogoro mkubwa kati ya waasi wanaoungwa mkono na Iran na vikosi vinavyomtii rais aliyekimbilia uhamishoni Saudi Arabia mwezi Februari, Abedrabbo Mansour Hadi.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/afp
Mhariri:Josephat Charo